Chilambo, Nashon watema cheche Simba

DAR ES SALAAM: WALA hawakutaka kupoteza muda. Ndivyo unavyoweza kuelezea mwanzo wa safari ya nyota wapya wa Simba, Nathaniel Chilambo na Kelvin Nashon, ambao wameanza kuonesha uwezo wao katika mazoezi ya kikosi hicho huku wakijitosa kuwania nafasi katika kikosi cha kwanza.
Chilambo na Nashon ni miongoni mwa wachezaji wapya waliotambulishwa na Simba katika dirisha hili la usajili na tayari wameungana na wenzao kambini kwa maandalizi ya msimu mpya pamoja na michuano ya CECAFA.

Kocha Msaidizi wa Simba, Seleman Matola, amesema ameridhishwa na hali ya kikosi tangu kilipoanza mazoezi, akibainisha kuwa wachezaji wengi walirejea katika kiwango kizuri baada ya kufuata programu za mazoezi walizopewa wakati wa mapumziko.
“Tunawapongeza wachezaji kwa sababu kabla ya mapumziko tuliwapa programu za kufanya nyumbani na wameirejea vizuri. Hilo limetupa picha nzuri tangu siku ya kwanza ya mazoezi,” amesema Matola.
Aliongeza kuwa hata wachezaji wapya wameonesha kuzoea mazingira haraka na hawakuonekana kama wageni katika kipindi cha kwanza cha mazoezi.
“Kwanza tulifanya vipimo vya utimamu wa mwili ili kuona kila mmoja yupo katika hali gani. Matokeo yanaonesha wamerudi katika hali nzuri kabisa, hivyo tumeendelea na programu yetu ya maandalizi pamoja na mazoezi ya kiufundi kama tulivyokuwa tumepanga,” amesema.




