Kwingineko

Dwayne Johnson: Nilikatishwa tamaa kabla ya kuanza kuigiza

CALIFORNIA: Mmoja wa mastaa wakubwa wa filamu duniani, Dwayne Johnson, amefichua kuwa mwanzoni mwa safari yake ya uigizaji huko Hollywood alikumbana na upinzani mkubwa, huku baadhi ya watu wakimtaka aachane na ndoto za uigizaji huku wakimtaka aendelee na mchezo wa mieleka.

Johnson, anayejulikana pia kwa jina la ‘The Rock’, amesema wakati alipoweka wazi azma yake ya kuwa muigizaji, alionya kuwa mashabiki hawangemkubali nje ya ulingo wa mieleka.

Alieleza kwamba wapo waliomshauri kuwa angeendelea kufanya vizuri zaidi kama mwanamieleka kuliko kujaribu bahati yake kwenye tasnia ya filamu.

Licha ya maneno hayo ya kukatisha tamaa, nyota huyo hakurudi nyuma. Aliamua kusimamia ndoto zake na kujitosa Hollywood, ambako baadaye alipata nafasi katika filamu kadhaa zilizofanya vizuri kimataifa na kujijengea jina kama mmoja wa waigizaji wanaovutia watazamaji wengi duniani.

Kutokana na mafanikio hayo, Johnson amegeuka kuwa miongoni mwa waigizaji wanaolipwa mamilioni ya dola kwa kila filamu, huku pia akifanikiwa kama mtayarishaji na mfanyabiashara. Safari yake imekuwa mfano kuwa kuamini uwezo wako na kupuuza maneno ya kuwakatisha tamaa kunaweza kufungua milango ya mafanikio makubwa.

Kauli ya Johnson imezua hisia mbalimbali miongoni mwa mashabiki wake, wengi wakisema simulizi lake ni somo muhimu kwa vijana wanaotamani kutimiza ndoto zao, wakisisitiza kuwa mafanikio hayapatikani kwa kuwasikiliza wanaokukatisha tamaa, bali kwa kufanya kazi kwa bidii na kuamini maono yako.

Related Articles

Back to top button