Nyumbani

Hamad Furahisha atamba kumchapa Patrick

DAR ES SALAAM: Bondia Hamad Furahisha, maarufu kwa jina la Mfupa wa Sokwe, ametamba kuwa atamfunza adabu mpinzani wake John Patrick katika pambano la Dar Boxing Derby litakalofanyika Julai 24, 2026, Ubungo jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati akiendelea na maandalizi ya pambano hilo nyumbani kwake Yombo Dovya, Temeke, Furahisha amesema wapinzani wake wamefanya makosa kumchagua John Patrick kwani anaamini ataondoka ulingoni akiwa amepokea kipigo kitakachomfanya achukie mchezo wa ngumi.

“Nitampa kipigo kikubwa kuliko kile nilichompa Enock Phiri wa Malawi. Waliomtuma wamemponza, safari hii ataona ubora wangu ulingoni,” amesema Furahisha.

Kocha wake, Haji Pera, amesema maandalizi yamekamilika na bondia huyo, yuko katika kiwango bora, akisisitiza kuwa wamejipanga kuhakikisha ushindi unapatikana bila kuacha nafasi ya mshangao.

Naye meneja wa bondia huyo, Habibu Othumani ‘Big’, amesema wana imani kubwa na Furahisha kutokana na maandalizi aliyofanya, huku akiwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi kushuhudia pambano hilo.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, Rashid Mbaga, amesema watanunua tiketi kwa baadhi ya wakazi na kuwaandalia usafiri wa kwenda na kurudi kutoka ukumbini ili kuongeza hamasa kwa mwakilishi wao.

Diwani wa Kata ya Makangarawe, Fadhili Mboga, amewataka wananchi wa Temeke kujitokeza kwa wingi kuonesha mshikamano kwa bondia huyo, akieleza kuwa ushindi wake utakuwa fahari kwa eneo zima.

Mbali na pambano hilo, mabondia wengine watakaopanda ulingoni siku hiyo ni Juma Choki na Tony Rashidi, ambapo mshindi ataondoka na gari aina ya Toyota Rumion.
Mwisho

Related Articles

Back to top button