Kingo: Tasnia ya filamu, tamthilia yahitaji kuungwa mkono

DARE ES SALAAM: Mchora katuni maarufu na muigizaji wa tamthilia mbalimbali nchini, Abdul Kingo, amesema tasnia ya filamu na tamthilia nchini inaendelea kupiga hatua kubwa za maendeleo, lakini inahitaji kuungwa mkono na wadau mbalimbali ili kufikia malengo ya kukuza ubora, ajira na ushindani katika soko la ndani na kimataifa.
Abdul Kingo alitoa kauli hiyo alipotembelea banda la TSN katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), akieleza kuwa maendeleo yanayoonekana kwa sasa ni matokeo ya juhudi za wasanii, waandaaji na wadau wa sekta hiyo, hivyo kuna umuhimu wa kuongeza uwekezaji na ushirikiano ili sanaa hiyo iwe kimbilio la mafanikio kwa wasanii na wadau kwa ujumla.
Alisema kuwa sekta ya filamu na tamthilia imeendelea
kutoa fursa za ajira kwa vijana wengi pamoja na kuitangaza Tanzania kupitia kazi za ubunifu, hivyo ni wakati wa Serikali, sekta binafsi na wadau wengine kushirikiana kuifanya tasnia hiyo iwe yenye kuleta matunda mazuri kwa wote.
Aidha, Abdul Kingo aliwataka Watanzania kuendelea kuunga mkono kazi za wasanii wa ndani kwa kuzitazama na kuzithamini, akisisitiza kuwa hatua hiyo itachochea ukuaji wa tasnia na kuwapa hamasa wabunifu kuendelea kuzalisha kazi zenye ubora wa kimataifa.




