Her Initiative kujengea ujuzi wanawake 50

DAR ES SALAAM: Shirika la Her Initiative limechagua wanawake vijana 50 kujiunga na programu ya Panda Academy inayolenga kuwajengea uwezo wa kubadili bidhaa na vipaji vyao kuwa biashara zenye chapa imara, ushindani na uwezo wa kukua katika soko.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Her Initiative, Lydia Charles Moyo, amesema wanawake wengi wana vipaji vya kuzalisha bidhaa bora na kutoa huduma zenye ubora, lakini hukosa fursa za kuzigeuza kuwa biashara za urembo zenye ushindani
“Programu hiyo ya miezi sita inalenga kuwawezesha washiriki kwa mafunzo ya maendeleo ya biashara, ujasiriamali, uongozi na fursa za masoko ili kuwasaidia kujenga biashara endelevu na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Tanzania.
“Kupitia mkakati unaozingatia haki (Rights-Based Approach) na mahitaji halisi ya soko, Panda Academy itawapatia washiriki ujuzi wa kiufundi, usimamizi wa biashara, ujenzi wa chapa na mbinu za kuongeza ushindani wa biashara zao.
Amesema Wanawake hao 50 wamepatikana baada ya mchakato wa ushindani uliowahusisha waombaji wengi kupitia usaili wa vitendo na mahojiano. Katika kipindi cha mafunzo watabobea katika utengenezaji wa kucha, bidhaa za ngozi, urembo na vipodozi pamoja na utengenezaji wa manukato.
Takwimu za Her Initiative zinaonyesha kuwa Panda Academy tayari imewawezesha zaidi ya wanawake vijana 210 kuanzisha na kukuza biashara katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo biashara, huduma za upishi, utengenezaji wa sabuni, mapambo ya ndani na biashara za urembo.
Mwanzilishi wa Her Initiative, Lydia Charles Moyo, amesema wanawake wengi wana vipaji vya kuzalisha bidhaa bora na kutoa huduma zenye ubora, lakini hukosa fursa za kuzigeuza kuwa biashara zenye ushindani kutokana na changamoto za mitaji, masoko, ujenzi wa chapa, uzingatiaji wa sheria na ukosefu wa ushauri wa kitaalamu.
Amesema Panda Academy ilianzishwa kuziba pengo hilo kwa kuwapatia vijana wanawake mfumo unaowawezesha kujenga biashara zenye ushindani na ukuaji wa muda mrefu.
“Kadri programu ilivyokuwa ikikua, tumegundua kuwa msaada unaolenga sekta maalumu huleta matokeo bora zaidi. Mwaka huu tumeamua kuwekeza katika sekta ya urembo kwa kuwa ni miongoni mwa sekta zinazokua kwa kasi na zenye fursa kubwa kwa wanawake vijana,” amesema Moyo.
Ameongeza kuwa dhamira ya Her Initiative si kuwajengea wanawake biashara pekee, bali kujenga kampuni zinazozalisha kipato, kutengeneza ajira, kuimarisha viwanda vya ndani na kuchangia maendeleo ya uchumi wa taifa.
Kiongozi wa Mradi wa Panda Academy, Nancy Faustine, alisema washiriki watatumia mwongozo unaowawezesha kujifunza ujuzi wa vitendo, kujenga biashara endelevu na kuwa viongozi katika familia, biashara na jamii.
Amesema mafunzo hayo yatahusisha maendeleo ya biashara na ujasiriamali, ujenzi wa chapa na ufungashaji, usimamizi wa fedha na upangaji wa bei, masoko ya kidijitali, urasimishaji wa biashara, uzingatiaji wa sheria na viwango, ushauri elekezi kutoka kwa wataalamu pamoja na maandalizi ya kuingia sokoni kupitia maonesho ya biashara.
Naye Mkufunzi wa Panda Academy, Vaileth Siyanga, amesema vijana wengi tayari wana vipaji, lakini hukosa mfumo wa kuvigeuza kuwa biashara zenye ushindani.
“Tunawafundisha washiriki kufikiria zaidi ya kutengeneza bidhaa. Wanajifunza kujenga chapa zinazoaminika, kuelewa mahitaji ya wateja, kupanga bei kwa usahihi, kuzingatia viwango vya ubora na kujenga biashara zinazoweza kukua kwa muda mrefu,” amesema Siyanga.



