‘Thank you’ yatua sebuleni kwa Chilunda
DAR ES SALAAM: KATIKA kuendelea kufanya maboresho ya kikosi cha timu hiyo, uongozi wa Simba umetangaza kuachana na mshambuliaji wake mzawa Shaban Chilunda baada ya mkataba wake kufikia tamati.
Imeelezwa kuwa Waziri Junior yupo kwenye rada za kutakiwa na Simba ambayo ipo katika mchakato wa kuongeza mshambuliaji mzawa baada ya kuachana na Chilunda na John Bocco ambaye kwa sasa ni kocha wa timu ya vijana ya Simba.
Waziri ameanza kujadiliwa kuitumikia klabu hiyo kwa nafasi ya mshambuliaji mzawa baada ya kuonyesha kiwango kizuri alipokuwa KMC FC msimu uliomalizika akimaliza na mabao 11.
Katika mazungumzo na Spotileo, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema Chilunda amemaliza mkataba wake wa mwaka mmoja na hatakuwa sehemu ya kikosi cha Simba kaa msimu wa 2024/25.
Ahmed amemtaja Chilunda kama mchezaji kijana mwenye kiwango kizuri huku mchezaji huyo akijiunga na Simba kwa mkataba wa mwaka mmoja wenye nafasi ya kuongezewa endapo wangeridhishwa na kiwango chake.
“Kipindi cha dirisha la mwezi Januari Chilunda alicheza kwa mkopo KMC hadi mwisho wa msimu lakini sasa hayupo kwenye mipango ya timu kuelekea msimu ujao”.
“Simba inaamini katika uwezo wa nyota huyo na inamtabiria kufanya makubwa katika timu ambayo itamsajili, hna kuachwa kwake ni sehemu ya maboresho ya kikosi kwa msimu ujao,” amesema Ahmed.
Amesema baada ya kukamilika kwa mchakato wa kuwapa ‘Thank you ‘, wachezaji hao, watakuja kuweka wazi waliongezewa mikataba na mwisho watawatambulisha silaha zao mpya zilizosajiliwa kuanza kazi msimu ujao.
“Wanasimba watulie viongozi wanafanya usajili mkubwa kulingana na mahitaji ya timu yetu pamoja na mapendekezo ya benchi la ufundi kujenga Simba imara na bora,” amesema Ahmed.
Chilunda ni mchezaji wa tatu kupewa ‘Thank You’ baada ya John Bocco na Said Ntibazonkiza kutokuwa sehemu ya kikosi cha Simba kwa msimu wa 2024/25.