Nyumbani

Mwarobaini waja ishu ya kina Kagoma

DAR ES SALAAM: MWENYEKITI wa Kamati ya Sheria na hadhi za wachezaji, Said Soud amesema wanakuja na njia mpya ya kuondoa sintofahamu ya mikataba kwa klabu na wachezaji.

Amesema wanapokea malalamiko kutoka kwa wachezaji wa kike kuhusu kiwango cha fedha wanacholipwa lakini mengi ni uvunjaji wa mikataba kwa jumla (Wanawake na wanaume).

“Kila msimu tunapokea  kesi nyingi za mikataba kutoka soka la wanawake na wanaume hasa wanaume ikiwemo mvutano wa  kiwango kidogo cha fedha, hii inatokana na klabu kunufaika au wachezaji hao kutojua haki zao na elimu ya mikataba wanayoingia,” amesema.

Baadhi ya kesi hizo ikiwemo Prince Dube mchezaji wa Yanga alikuwa na mgongano na  Azam FC, Lameck Lawi kutoka Coastal Union kwenda Simba na hatimaye kumalizana kiungwana na kubaki Coastal.

Wachezaji wengine ni Yusuph Kagoma ambaye kwa sasa anatumikia Simba akitokea  Fountain Gate FC lakini kulikuwa na sintofahamun kati ya Yanga wakidai ni mchezaji wao halali na Awesu Awesu kutoka KMC FC kwenda Simba.

Soud amesema katika kutetea haki na kulinda ustawi wa wachezaji wote wapo na mpango wa kutoa elimu ya kisheria  kwa viongozi pamoja na wachezaji kuelezwa juu ya haki zao wanapokuwa katika makubaliano rasmi.

“Kwa kuwa tuko kwenye mpango huo, tumeanza kuzungumza na bodi ya ligi na TFF wanaoendesha ligi ili kukaa na viongozi wa klabu na wachezaji kuwapa elimu na wachezaji kusimama imara katika kutambua ustawi wao kwenye makubaliano,” amesema.

Related Articles

Back to top button