Ahoua, Belouizdad wapeana mkono wa kwaheri

ALGIERS: RASMI klabu ya CR Belouizdad ya Algeria imethibitisha kuachana na kiungo mshambuliaji wa Ivory Coast, Jean Charles Ahoua.
Belouizdad imetangaza kuachana na Ahoua kupitia majukwaa yake ya mitandao ya kijamii baada ya pande hizo mbili kufikia makubaliano ya kuvunja mkataba.
Taarifa zaidi zinafafanua kuwa Ahoua ameondoka baada ya kutoridhishwa na mazingira ya timu hiyo tangu kuondoka kwa aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Sead Ramović.
Naye, Ahoua kupitia ukurasa wake wa Mtandao wa Instagram, aliandika: “Niwashukuru Belouizdad, viongozi, benchi la ufundi, wachezaji wenzangu na mashabiki kwa uzoefu huu. Naitakia klabu kila la heri.”
Ahoua anayetajwa kuwa na thamani ya Pauni 275,000 kwa sasa, alitua Belouizdad Januari, mwaka huu akitokea Simba SC alikodumu kwa msimu mmoja na nusu, akionesha kiwango cha kuvutia.
Fununu zinafafanua kuwa kiungo huyo ambaye yuko huru, anatarajiwa kufanya uamuzi wa mwisho kuhusu hatimaye yake na klabu mpya atakayojiunga nayo katika siku za usoni.




