World Cup

Ufaransa, Morocco mechi ya kibabe Leo

BOSTON: Ufaransa na Morocco zinakutana leo katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la Dunia 2026 utakaopigwa kwenye Uwanja wa Boston Stadium, Foxborough, Marekani, huku kila timu ikisaka tiketi ya kufuzu nusu fainali.

Ufaransa ni miongoni mwa timu zinazopewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa, imekuwa katika kiwango bora baada ya kushinda michezo yake yote mitano na kufunga mabao 14 huku ikiruhusu mawili pekee.

Nahodha na mshambuliaji wa Ufaransa, Kylian Mbappe, anaongoza mbio za kuwania kiatu cha dhahabu akiwa amefunga mabao saba na kutoa pasi mbili za mabao. Mbali na Mbappe, timu hiyo pia inategemea uwezo wa Ousmane Dembele, Michael Olise na Bradley Barcola.

Morocco, bingwa wa Afrika, imeendelea kuthibitisha ubora wake baada ya kuziondoa Uholanzi na Canada katika hatua za mtoano na sasa inalenga kufika nusu fainali ya Kombe la Dunia kwa mara ya pili mfululizo.

Hata hivyo, kocha wa Morocco Mohamed Ouahbi amepata pigo baada ya mshambuliaji Ismael Saibari, ambaye amefunga mabao matatu kwenye mashindano haya, kukosekana kutokana na jeraha la misuli ya nyama ya paja (hamstring). Nafasi yake inatarajiwa kuchukuliwa na Soufiane Rahimi.

Kwa upande wa Ufaransa, kiungo Aurelien Tchouameni anaendelea kuwa na mashaka ya kucheza kutokana na majeraha ya misuli, ingawa kocha Didier Deschamps ana matumaini ya kuwa na kikosi chake bora.

Kwa mujibu wa takwimu za Opta, Ufaransa ina nafasi ya asilimia 61.7 ya kushinda ndani ya dakika 90, huku Morocco ikipewa asilimia 16.2 na uwezekano wa mchezo kwenda muda wa nyongeza ukiwa asilimia 22.1.

Mshindi wa mchezo huo atakutana na mshindi wa robo fainali nyingine kati ya Hispania na Ubelgiji katika hatua ya nusu fainali itakayochezwa Julai 14 mjini Dallas, Texas.

 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button