
NEW JERSEY: Huenda isiwe simulizi tamu kwa masikio ya wapenda soka duniani kote, lakini huo ndio ukweli. Nyota aliyebebeshwa matumaini makubwa tangu ujana wake, Neymar da Silva Santos Júnior, ameucheza mchezo wake wa mwisho katika historia ya michuano ya Kombe la Dunia.
Kutoka kwa kijana aliyeushangaza ulimwengu kwa kipaji chake cha kipekee, hadi kuwa mfungaji bora wa muda wote wa timu ya taifa ya Brazil, Neymar ameandika historia ambayo itadumu kwa vizazi.
“Nilijaribu. Nilijaribu. Safari yangu ilianza hapa, katika Uwanja wa MetLife, na sasa ndiyo nimeihitimisha hapa,” alisema Neymar baada ya mchezo dhidi ya Norway, wakifungwa mabao 2-0.
Katika safari yake ya Kombe la Dunia, alishiriki michuano minne tofauti, akiwapa mashabiki sababu ya kutabasamu kupitia kila chenga, kila pasi na kila bao. Ingawa hakuwahi kuinua kombe hilo, aliifanya jezi ya Brazil iendelee kuogopwa na kuheshimika kila alipokanyaga nyasi.
Leo, pazia linashuka kwa mmoja wa wanasoka wenye kipaji cha kipekee kuwahi kutokea katika kizazi hiki. Urithi wake hautapimwa kwa makombe pekee, bali kwa furaha, burudani na msukumo aliouacha kwa mamilioni ya wapenda soka duniani.




