Familia

Dayna Nyange ajivunia binti yake, akumbushia maumivu

MOROGORO: Msanii mkongwe wa muziki wa Bongo Fleva, Dayna Nyange, ameonesha furaha na shukrani baada ya binti yake, Rahma, kufaulu mtihani wa Kidato cha Sita kwa Daraja la Kwanza katika tahasusi ya Fizikia, Kemia na Baiolojia (PCB).

Kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, Dayna amesema mafanikio hayo ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu na matokeo ya juhudi za binti yake, huku akieleza kuwa safari ya malezi imejaa changamoto nyingi ambazo mara nyingi wazazi huzipitia kimya kimya.

Amesema wazazi wengi hubeba maumivu, hofu na machozi bila watu wengine kuyafahamu, lakini mwisho wa yote Mungu huandika hadithi nzuri kwa wale wanaoendelea kuwa na imani.

Dayna amesema hakuna furaha kubwa kwa mzazi kama kumuona mtoto wake akifanikiwa na kupiga hatua katika maisha, akieleza kuwa siku hiyo imejaa baraka, shukrani na furaha kwa mema ambayo Mungu ametenda katika familia yake.

Akimpongeza binti yake, amesema anajivunia mafanikio hayo na anaamini safari mpya ya kutimiza ndoto ya kuwa daktari imeanza.

“Hakika namshukuru Mungu kwa mafanikio haya na ninajivunia sana binti yangu. Asante Rahma kwa kuendelea kunifanya nijivunie. Tuna daktari wetu wa familia,” aliandika Dayna.

Aidha, amemtakia Rahma ulinzi, hekima na mafanikio zaidi katika hatua inayofuata ya masomo yake, akimuombea Mungu aendelee kumwongoza na kumbariki katika safari yake ya elimu.

Related Articles

Back to top button