BMT yatafuta fursa Paris za ushirikiano

PARIS: KATIBU Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha, ametembelea Taasisi ya Taifa ya Utaalamu na Uendelezaji Bora wa Michezo ya Ufaransa (INSEP) kwa lengo la kutafuta fursa za ushirikiano zitakazowezesha kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji vya michezo pamoja na kuboresha matokeo ya wanamichezo wa Tanzania.
INSEP ni taasisi yenye mchango mkubwa katika kuandaa na kutekeleza sera za michezo ya ushindani wa kiwango cha juu nchini Ufaransa.
Taasisi hiyo inatoa huduma mbalimbali zinazowawezesha wanamichezo kufikia mafanikio makubwa, ikiwemo programu za mafunzo zinazozingatia mahitaji ya kila mwanamichezo, huduma za tiba na afya ya michezo, tafiti za kisayansi, ushauri wa kisaikolojia, pamoja na elimu na maandalizi ya taaluma mbadala baada ya maisha ya ushindani.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Msitha amesema uwezo mkubwa wa INSEP umeonesha fursa nyingi ambazo BMT inaweza kuzitumia kupitia ushirikiano katika maeneo ya tafiti za michezo, kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji, pamoja na kuimarisha mifumo ya maendeleo ya michezo nchini Tanzania.
Naye Mkurugenzi wa INSEP, Babak Amir-Tahmasser, OLY, amesema taasisi hiyo ipo tayari kushirikiana na BMT katika maeneo mbalimbali ya kimkakati kwa kutumia uzoefu na utaalamu wake katika kuendeleza sekta ya michezo.
Aidha, Mkuu wa Miradi ya Kimataifa wa INSEP, Sean Gandrille, alimtembeza Msitha na kumuonesha miundombinu ya kisasa ya mafunzo yenye viwango vya kimataifa inayotumiwa kuwaandaa wanamichezo wa kiwango cha juu.




