Ronaldo kuibeba Ureno leo?

ARLINGTON: Macho ya dunia leo yataelekezwa kwenye Uwanja wa Dallas, Arlington, Marekani, ambako Ureno na Hispania zitamenyana katika hatua ya 16 Bora ya Kombe la Dunia 2026 kwenye pambano linalotarajiwa kuwa kali kutokana na ushindani wa muda mrefu kati ya mataifa hayo jirani.
Mchezo huo utaweka uso kwa uso nyota mkongwe Cristiano Ronaldo wa Ureno na kinda mwenye kipaji kikubwa Lamine Yamal wa Hispania katika pambano linalotajwa kuwa vita ya vizazi viwili tofauti.
Ureno ilifika hatua hiyo baada ya kumaliza nafasi ya pili Kundi J ikiwa na pointi tano, kabla ya kuiondoa Croatia kwa ushindi wa mabao 2-1 katika hatua iliyopita.
Hispania, kwa upande wake, iliongoza Kundi H kwa pointi saba na baadaye kuifunga Austria mabao 3-0 na kusonga mbele ikiwa haijapoteza mchezo wowote katika mechi zake 34 zilizopita.
Kwa Ronaldo mwenye umri wa miaka 41, mchezo huo unaweza kuwa hatua nyingine muhimu katika safari yake ya mwisho ya Kombe la Dunia, huku kukiwa na taarifa kuwa huenda akastaafu soka la kimataifa baada ya mashindano hayo.
Nahodha huyo tayari amefunga mabao matatu kwenye michuano hiyo, lakini bado anatamani kutwaa taji pekee ambalo halipo kwenye mkusanyiko wake wa mafanikio.
Kwa upande wa Hispania, Yamal amesema timu yao haina hofu na mpinzani yeyote na inaamini inaweza kufika mbali zaidi katika mashindano hayo. Kijana huyo mwenye miaka 18 ameendelea kung’ara, huku mshambuliaji Mikel Oyarzabal akiongoza kwa mabao manne.
Takwimu za Opta zinaipa Hispania nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi ndani ya dakika 90 kwa asilimia 49.2, wakati Ureno ikipewa asilimia 25.6, huku uwezekano wa mchezo kwenda muda wa nyongeza ukiwa asilimia 25.2.
Mshindi wa pambano hilo atatinga robo fainali ambako atakutana na mshindi kati ya Marekani na Ubelgiji.




