Kwingineko

Hat-trick YA Messi ilivyomtoa machozi KOCHA SCALONI

MISSOURI:KOCHA wa Argentina Lionel Scaloni alishindwa kuficha hisia zake baada ya Lionel Messi kufunga hat-trick na kuiongoza Argentina kupata ushindi muhimu katika Kombe la Dunia.

Kocha huyo alionekana akiwa na machozi baada ya mechi, picha iliyogusa mashabiki wengi wa soka duniani na kuonesha uhusiano mkubwa uliopo kati yake na nahodha huyo wa Argentina.
Safari ya wawili hao imekuwa ya kipekee tangu mwaka 2018, baada ya Argentina kufanya vibaya katika Kombe la Dunia nchini Urusi. Wakati huo, Scaloni aliteuliwa kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Argentina licha ya upinzani mkubwa kutoka kwa mashabiki na wachambuzi wengi wa soka waliodhani hakuwa na uzoefu wa kutosha kwa kazi hiyo.
Miaka yake ya mwanzo haikuwa rahisi. Aliendelea kukosolewa mara kwa mara, lakini ndani ya kipindi hicho alikuwa akijenga timu mpya yenye mfumo ambao ungemruhusu Messi kucheza kwa uhuru zaidi.
Lengo lake halikuwa kuifanya Argentina imtegemee Messi pekee, bali kuunda kikosi ambacho kingemsaidia nyota huyo kuonesha uwezo wake bila kubeba mzigo wote wa timu mabegani mwake.
Wakati huo pia Messi alikuwa ametoka kupitia vipindi vigumu akiwa na timu ya taifa, hadi kufikia hatua ya kuwahi kufikiria kustaafu soka la kimataifa kutokana na presha na ukosoaji aliokuwa akipokea.
Hata hivyo, kuwasili kwa Scaloni kulibadilisha mambo mengi. Chini ya uongozi wake, Argentina ilianza kurejea kwenye ubora wake na kuvunja ukame wa miaka 28 bila taji kubwa.
Katika kipindi hicho, Argentina imefanikiwa kutwaa Copa America 2021, Finalissima 2022,Kombe la Dunia 2022 na Copa America 2024
Mafanikio hayo yameifanya Argentina kurejea kileleni mwa soka la dunia, huku Scaloni akitajwa kuwa mmoja wa makocha walioleta mapinduzi makubwa zaidi katika historia ya timu hiyo.
Leo hii, wawili hao wamebaki kuwa sehemu muhimu ya historia ya Argentina, watu waliobadilisha mwelekeo wa taifa hilo na kurejesha ndoto za mamilioni ya mashabiki wa Albiceleste duniani kote.

Related Articles

Back to top button