Kwingineko

Aliyeacha kazi benki na kutimiza ndoto ya Kombe la Dunia

ATLANTA:WAKATI timu ya taifa ya Cape Verde ikiwa imeshacheza mechi yake ya kwanza ya Kombe la Dunia 2026, mmoja wa wachezaji waliovutia wengi ni beki Roberto Carlos Lopes, ambaye safari yake ya soka imejaa maamuzi makubwa na ya kishujaa.

Roberto Carlos Lopes, aliyezaliwa na kukulia nchini Ireland, aliwahi kuwa mfanyakazi wa benki akiwa na umri wa miaka 24. Wakati huo alikuwa na ajira ya kudumu katika moja ya benki nchini humo, huku akiichezea klabu ya Bohemians kama mchezaji wa muda.

Licha ya kuwa na maisha yaliyokuwa yanaonekana kuwa salama na yenye uhakika, moyo wake ulikuwa bado kwenye soka. Mwaka 2017 alipata ofa kutoka klabu ya Shamrock Rovers iliyomtaka aachane na kazi yake ya benki na kuwa mchezaji wa kulipwa moja kwa moja.

Uamuzi huo haukuwa rahisi. Watu wengi walimshauri aendelee na ajira yake benki, lakini Lopes aliamua kufuata ndoto zake. Akaacha kazi na kujiunga na Shamrock Rovers, hatua ambayo baadaye ilibadili kabisa maisha yake.

Miaka michache baadaye, alikumbana na tukio la kipekee. Kocha wa timu ya taifa ya Cape Verde wa wakati huo, Rui Aguas, alimtumia ujumbe kupitia LinkedIn akimualika kujiunga na timu ya taifa ya nchi ya asili ya baba yake.

Tatizo lilikuwa kwamba ujumbe huo uliandikwa kwa lugha ya Kireno, lugha ambayo Lopes hakuifahamu. Kutokana na hilo, hakujibu chochote. Miezi nane baadaye kocha huyo alimtumia tena ujumbe mwingine, ndipo alipoamua kuutafsiri kwa kutumia mtandao na kugundua kuwa alikuwa amealikwa kuichezea Cape Verde.

Ingawa aliwahi kuchezea timu za vijana za Ireland, mwaka 2019 aliamua kuikubali Cape Verde na kuanza safari mpya ya kimataifa.

Leo, miaka kadhaa baadaye, uamuzi wake umezaa matunda makubwa. Lopes amekuwa sehemu muhimu ya safu ya ulinzi ya Cape Verde na amesaidia taifa hilo kuandika historia kwa kufuzu Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza.

Kutoka ofisini benki hadi kwenye jukwaa kubwa zaidi la soka duniani, safari ya Roberto Carlos Lopes ni ushahidi kuwa wakati mwingine mafanikio makubwa huanza pale unapothubutu kuacha njia iliyo salama na kufuata ndoto unayoamini.

Related Articles

Back to top button