Serikali kupunguza ada za Leseni za maudhui mtandaoni

DODOMA:WAZIRI wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, amesema Serikali inapendekeza kupunguza kwa kiwango kikubwa ada mbalimbali za leseni za maudhui mtandaoni zinazotumiwa zaidi na vijana, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya biashara na kuharakisha ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini.
Akiwasilisha Bungeni mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Waziri Khamisi amesema marekebisho hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara Nchini (MKUMBI) pamoja na jitihada za kuondoa vikwazo vinavyokwamisha maendeleo ya sekta mbalimbali.
Ameeleza kuwa Serikali inapendekeza kufanya marekebisho katika Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui Mtandaoni) kwa kupunguza ada zinazohusiana na leseni za maudhui mtandaoni ili kuongeza ushiriki wa wananchi, hususan vijana, katika shughuli za uchumi wa kidijitali.
Kwa mujibu wa mapendekezo hayo, ada ya maombi ya leseni ya huduma za maudhui mtandaoni itapunguzwa kutoka Sh. 50,000 hadi Sh. 10,000. Aidha, ada za mwanzo, za mwaka na za kuhuisha leseni hiyo zitashushwa kutoka Sh.500,000 hadi Sh. 50,000.
Vilevile, Serikali inapendekeza kupunguza ada ya maombi ya leseni ya mtengeneza maudhui mtandaoni (Online Content Aggregator) kutoka Sh. 100,000 hadi Sh. 20,000. Ada za mwanzo, za mwaka na za kuhuisha leseni hiyo nazo zitapunguzwa kutoka Sh. 1,000,000 hadi Sh. 100,000.
Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza fursa kwa wabunifu wa maudhui mtandaoni, kuvutia uwekezaji zaidi katika sekta ya kidijitali na kuchangia ukuaji wa uchumi unaotegemea teknolojia nchini.



