Mwakinyo kuwania mkanda wa IBO

DAR ES SALAAM: BONDIA nyota wa Tanzania, Hassan Mwakinyo, anatarajiwa kupanda ulingoni Juni 10, 2026 nchini Ivory Coast kumenyana na bondia wa Ufaransa, Michel Soro, katika pambano la kuwania mkanda wa dunia wa International Boxing Organization wa uzani wa Middleweight.
Pambano hilo litafanyika katika ukumbi wa Abidjan Arena na linatarajiwa kuvuta hisia za mashabiki wa ngumi kutokana na ubora na rekodi za mabondia hao wawili.
Mwakinyo anaingia katika pambano hilo akiwa na rekodi ya kucheza mapambano 28 ya kulipwa, akishinda 25 na kupoteza matatu.
Kwa upande wake, Soro amepigana mapambano 44, akishinda 38, kupoteza manne na kutoka sare mara mbili, jambo linaloonesha uzoefu mkubwa alionao bondia huyo wa Ufaransa.
Pambano hilo linatajwa kuwa moja ya mapambano makubwa katika maisha ya Mwakinyo, ambaye amekuwa akiendelea kujiimarisha katika ngazi ya kimataifa kwa lengo la kutwaa mataji makubwa ya dunia.
Mara ya mwisho Mwakinyo kupanda ulingoni ilikuwa mwezi Desemba mwaka jana alipomshinda Stanley Eribo wa Nigeria, ushindi uliompa ari na kuimarisha nafasi yake kuelekea pambano hilo la ubingwa wa dunia.




