Slot: Nimeiacha Liverpool ilipostahili

LONDON: ALIYEKUWA kocha mkuu wa Liverpool, Arne Slot, amesema anaondoka klabuni hapo akiwa na imani kuwa ameiacha katika nafasi yake sahihi miongoni mwa timu bora zaidi barani Ulaya baada ya kufutwa kazi mwishoni mwa wiki.
Kocha huyo raia wa Uholanzi mwenye umri wa miaka 47 alitoa kauli hiyo kupitia barua ya wazi aliyowaandikia mashabiki wa Liverpool, akieleza kuwa anajivunia mafanikio aliyoyapata akiwa Anfield licha ya kuondolewa kwenye nafasi yake.
Slot, ambaye alichukua mikoba ya Jurgen Klopp mwaka 2024, alianza vyema maisha yake Liverpool kwa kuiongoza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England katika msimu wake wa kwanza, lakini baadaye alifutwa kazi baada ya timu kumaliza nafasi ya tano msimu huu, ikiwa nyuma kwa pointi 25 dhidi ya mabingwa Arsenal.
“Ninaondoka nikiwa na imani kamili kuhusu mustakabali wa klabu hii. Wachezaji wamejenga msingi imara ambao utaendelea kudumu kwa muda mrefu,” amesema Slot.
Amesema kufuzu kwa Liverpool kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao ni moja ya mafanikio muhimu yaliyopatikana chini ya uongozi wake.
“Kuhakikisha Liverpool inacheza Ligi ya Mabingwa ilikuwa jukumu muhimu kwa sababu linatoa nafasi ya klabu kuendelea kushindana katika kiwango cha juu zaidi msimu ujao na miaka ijayo,” amesema.
Slot aliwashukuru mashabiki wa Liverpool kwa mapokezi mazuri aliyopata tangu siku ya kwanza alipowasili Anfield, akisema sapoti yao ilichangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya timu hiyo.
Alikumbuka kwa hisia ushindi wa ubingwa wa 20 wa ligi katika historia ya Liverpool, akisema kusherehekea mafanikio hayo pamoja na mashabiki kulifanya tukio hilo kuwa la kipekee zaidi.
Katika barua yake, Slot pia alimuenzi aliyekuwa mshambuliaji wa Liverpool, Diogo Jota, aliyefariki dunia katika ajali ya gari pamoja na ndugu yake Andre Silva mwaka jana.
Amesema namna mashabiki, wachezaji na familia nzima ya Liverpool walivyoungana katika kipindi hicho kigumu ni jambo ambalo hataweza kulisahau maishani mwake.
Wakati huo huo, Liverpool inatarajiwa kuanza mazungumzo rasmi na kocha wa zamani wa Bournemouth, Andoni Iraola, ambaye anatajwa kuwa miongoni mwa wanaopewa nafasi kubwa ya kurithi mikoba ya Slot.




