Class apata dili kufanya mazoezi nchini Marekani

DAR ES SALAAM: BONDIA wa Tanzania, Ibrahim Class, amesema amepokea kwa furaha kubwa kukubaliwa kwenda kufanya mazoezi chini ya bondia bingwa wa Marekani, Terence Crawford, akieleza kuwa hatua hiyo ni ndoto aliyokuwa akiisubiri kwa muda mrefu.
Akizungumza Dar es Salaam Class amesema nafasi hiyo ni mafanikio makubwa katika safari yake ya ngumi na itampa hamasa mpya ya kuendelea kukuza kipaji chake na kufikia mafanikio makubwa zaidi katika mchezo huo.
“Ilikuwa ni ndoto yangu kupata nafasi kama hii. Kukubaliwa kwenda kufanya mafunzo chini ya Crawford ni jambo kubwa sana kwangu na ninaamini litakuwa chachu ya maendeleo katika kazi yangu ya ubondia,” amesema Class.
Amefafanua kuwa mafunzo hayo yatamuwezesha kufanya kazi na makocha wenye uzoefu mkubwa wa kimataifa pamoja na kujifunza mbinu mpya zitakazomsaidia kuongeza uwezo wake na ushindani wake ulingoni.
Class amesema uzoefu atakaoupata nchini Marekani utakuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha kiwango chake na kufungua fursa zaidi katika maisha yake ya ubondia.
Takwimu za mtandao wa boxrec zinaonesha bondia huyo wa Marekani amecheza mapambano 42 na kushinda yote, hajapoteza wala kupata sare.
Mwisho




