Nsangazelu: Hatuendi Kombe la Dunia kinyonge

RABAT: KOCHA wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys, Elieneza Nsangazelu amesema ushindi walioupata dhidi ya Misri umeongeza imani kwa kikosi hicho kufanya makubwa zaidi katika michuano ya Kombe la Dunia.
Serengeti Boys ilitinga fainali baada ya kuiondosha Misri kwa mikwaju ya penalti 4-3 kufuatia sare tasa ndani ya dakika 90 za mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa.
Akizungumza baada ya ushindi huo, Nsangazelu amesema vijana wake wameonesha uwezo mkubwa na kuthibitisha kuwa hakuna jambo lisilowezekana wanapokuwa wamoja na kujituma.
“Ushindi huu umetupa imani kwamba hakuna jambo linaloshindikana. Tumeweza kufanya hapa na tunaweza kufanya hata zaidi huko mbele tunakoelekea,” amesema Nsangazelu.
Kocha huyo amesema sasa macho yao yapo kwenye michuano ya Kombe la Dunia kwa vijana ambapo wanaamini wataenda kupambana na kufanya vizuri badala ya kushiriki tu.
“Watanzania wajiandae kwa sababu hatutaenda kinyonge. Tutaenda kama wachezaji wakubwa wenye malengo ya kufanya vizuri na kuipeperusha vyema bendera ya taifa,” amesema.
Aidha, amewapongeza vijana wake kwa moyo wa kujituma na nidhamu waliyoonesha katika mashindano hayo huku akiwaomba Watanzania kuendelea kuwaunga mkono.
“Watanzania wanapaswa kujivunia vijana wao kwa kazi kubwa waliyoifanya. Muhimu ni kuendelea kuwapa sapoti kwa sababu bado wanawategemea,” amesema.
Nsangazelu ameongeza kuwa anaamini kwa msaada wa Mungu pamoja na ushirikiano kutoka kwa Watanzania, Serengeti Boys inaweza kufika mbali zaidi na kuandika historia mpya katika soka la vijana.




