Ligi Kuu

TRA ina nafasi ya kufanya vizuri – Mwagala

ARUSHA: OFISA Habari wa TRA United Christina Mwagala amesema sare waliyoipata dhidi ya JKT Tanzania ni matokeo yaliyowaumiza kutokana na kuhitaji pointi tatu muhimu, lakini bado wanaamini wana nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika michezo iliyosalia.

Mwagala amesema baada ya mchezo huo uliochezwa katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha kuwa matokeo hayo yanapaswa kubaki hapo huku wakielekeza nguvu kwenye michezo ijayo.

“Ni matokeo ya kutuumiza kwa sababu tulihitaji kupata pointi tatu, lakini huu ni mpira wa miguu na matokeo haya tunayaacha hapa Sheikh Amri Abeid,” amesema Mwagala.

Amesisitiza kuwa TRA United bado ipo kwenye nafasi nzuri ya kupambana ili kufuzu kushiriki michuano ya kimataifa kupitia ligi kuu.

Aidha amesema sare hiyo haipaswi kuwavunja moyo mashabiki wala kuwaondoa kwenye matumaini ya timu hiyo kufanya vizuri msimu huu.

“Sare hii isiwatoe kwenye mchezo wala isiwaumize kichwa, tuna michezo saba iliyobaki na yote iko ndani ya uwezo wetu, tuna nafasi kubwa ya kushinda,” amesema.

Mwagala ameongeza kuwa timu hiyo itaendelea kupambana kwa nguvu zote katika kila mchezo uliosalia kuhakikisha wanafikia malengo waliyojiwekea msimu huu.

“Popote tunapopita kwenye milima, bahari na miti tunapanda,” amesema kwa kujiamini.

Related Articles

Back to top button