Atletico yapata pigo jipya la majeruhi

MADRID:KLABU ya Atletico Madrid imeingia katika taharuki ya majeruhi kwa wachezaji wake muhimu kuelekea mchezo wa marudiano wa UEFA Champions League dhidi ya Arsenal.
Habari njema kwa kocha Diego Simeone ni kurejea salama kwa mshambuliaji Julian Alvarez aliyefunga bao katika mchezo wa jana dhidi ya Arsenal ambaye alionekana kupata maumivu ya kifundo cha mguu, lakini hakuumia vibaya.
Hata hivyo, Atletico imepata pigo kwa mshambuliaji Alexander Sorloth ambaye alikosa kabisa kucheza baada ya kupata majeraha ya msuli wa nyuma wa paja (hamstring) wakati wa mazoezi ya kupasha misuli joto.
Mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo alieleza kuwa Sorloth alikuwa bado hajapona kabisa baada ya kupata maumivu wiki iliyopita, na hali yake ilizidi kuwa mbaya wakati wa maandalizi ya mechi.
“Alikuwa ametulia kwa wiki moja baada ya maumivu ya nyuma ya paja, lakini alipofanya harakati za kawaida wakati wa kupasha misuli joto, hali ilirudi tena na kushindwa kucheza,” imeelezwa.
Wakati huo huo, kiungo Giuliano Simeone naye ameibua hofu baada ya kutolewa mapema kipindi cha kwanza kufuatia maumivu aliyoyapata kiunoni.
Simeone amesema ana tumaini majeraha hayo si makubwa, huku akisisitiza kuwa bado ana matumaini ya kuwaona wachezaji hao wakirejea kwa ajili ya mchezo wa pili ugenini.
Changamoto hizo zinaifanya Atletico kuwa katika wakati mgumu kabla ya kuivaa Arsenal, huku lengo likiwa ni kufuzu fainali ya michuano hiyo mikubwa barani Ulaya.




