Nyavu

DAREVA yajipanga kuboresha mzunguko wa pili wa Ligi

DAR ES SALAAM: BODI ya Ligi ya Chama cha Mpira wa Wavu Mkoa wa Dar es Salaam (DAREVA) imesema imeanza mikakati ya kufanya maboresho mbalimbali yatakayolenga kuupa ubora zaidi mzunguko wa pili wa ligi hiyo pamoja na kuongeza ushindani kwa timu shiriki.

Akizungumza kuhusu maandalizi hayo, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Peter Kahwaa, amesema maboresho yanayopangwa yatahusisha maeneo muhimu ikiwemo kanuni za ligi, uchezaji wa timu na uendeshaji wa waamuzi, ili kuhakikisha mashindano yanaendeshwa kwa kiwango cha juu na kwa ufanisi zaidi.

“Kupitia mzunguko wa pili, tunalenga kuboresha maeneo kadhaa ikiwemo kanuni, uchezaji wa timu pamoja na uamuzi, ili kuondoa changamoto ndogo ndogo zilizojitokeza na kuhakikisha ligi inaendeshwa kwa weledi mkubwa,” amesema Kahwaa.

Amesema kuwa hatua hiyo inalenga kupunguza makosa yanayoweza kuepukika wakati wa michezo na kuhakikisha kila kitu kinafuata taratibu na miongozo iliyowekwa na bodi hiyo.

Mbali na hilo, Kahwaa amebainisha kuwa DAREVA pia inalenga kuongeza mvuto wa ligi hiyo kwa mashabiki, ili kuendelea kuhamasisha ukuaji wa mpira wa wavu nchini ambao kwa sasa unaonesha dalili kubwa ya kupanda kwa kasi.

“Tunataka kuona mashabiki wengi zaidi wanajitokeza viwanjani na kuendelea kuupenda mchezo huu, kwani mpira wa wavu unakua kwa kasi na unahitaji sapoti ya wadau wote,” amesisitiza.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button