Presha yahamia Yanga Princess baada ya kuporomoka

DAR ES SALAAM: MBIO za ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara zimechukua sura mpya baada ya Yanga Princess kuanza kudondosha alama muhimu, kufuatia kuchapwa mabao 2-0 na Tausi katika mchezo wa mzunguko wa 13 uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Azam Complex.
Kupoteza huko kumeifanya Yanga Princess kuendelea kubaki nyuma ya vinara Simba Queens, ambao sasa wameongeza tofauti ya pointi hadi nne baada ya kufikisha pointi 37 kufuatia ushindi wao dhidi ya Bunda Queens katika mchezo wa ugenini uliochezwa kwenye Uwanja wa Karume mkoani Mara.
Kabla ya michezo ya jana, Yanga Princess walikuwa nyuma kwa pointi moja tu, lakini matokeo hayo sasa yanaifanya timu hiyo kuingia kwenye presha kubwa ya mbio za ubingwa, hasa ikizingatiwa kuwa bado haijawahi kutwaa taji la ligi hiyo.
Kwa upande wa Tausi Women, ushindi huo muhimu umeipa timu hiyo nguvu mpya baada ya kufikisha pointi 15 na kushika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi.
Katika michezo mingine ya jana, Ceasiaa Queens ilitoka sare tasa dhidi ya Alliance Girls kwenye Uwanja wa Samora mkoani Iringa, huku Mashujaa Queens ikiibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Ruangwa Queens kwenye Uwanja wa Kituo cha TFF Kigamboni.
Yanga Princess sasa wanalazimika kushinda michezo yao ijayo bila makosa ikiwa wanataka kuendelea kubaki kwenye mbio za ubingwa, ikiwaombea Simba kufanya vibaya mchezo mmoja au mwili jambo ambao huenda likawa gumu kwa kuwa nao Simba Queens wanazidi kuonekana kuutazama ubingwa kwa jicho la karibu zaidi.




