Atiki kuipambania Dar City kesho

PRETORIA, Afrika Kusini: DAR CITY itaanza rasmi safari yake ya kusaka mafanikio kwenye michuano ya Basketball Africa League (BAL) Kalahari Conference kesho, itakapomenyana na Johannesburg Giants nchini Afrika Kusini.
Mabingwa hao wa Tanzania wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa wamejipanga kuonesha ushindani mkubwa, huku wakiimarisha kikosi chao kwa kusajili wachezaji wenye uzoefu wa kimataifa.
Katika kujiandaa na michuano hiyo, Dar City imemtambulisha rasmi mchezaji wa kikapu wa Tanzania, Atiki Ally, ambaye kwa sasa anacheza kikapu cha kulipwa akiwa na klabu ya New Mexico nchini Marekani.
Atiki, ambaye kwa muda mrefu ameishi Marekani, aliwahi kupata ufadhili wa kusoma na kucheza mpira wa kikapu huko, jambo lililomjengea uzoefu mkubwa wa kimataifa unaotarajiwa kuwa msaada kwa Dar City katika mashindano hayo.
Mbali na Atiki, Dar City pia imeongeza nguvu kwa kuwasajili mastaa wengine wa kimataifa kwa ajili ya BAL Kalahari Conference, akiwemo David Michineau anayetokea AS Monaco, Junior Madut wa Sudan Kusini anayekipiga kwenye Ligi ya Kikapu ya Kosovo, pamoja na Nisre Zouzoua aliyejiunga na timu hiyo mwaka jana akitokea FUS Rabat ya Morocco.
Wengine waliopo kwenye kikosi hicho ni Michael Foster na Deng Junior, ambao wote wamewahi kucheza katika klabu mbalimbali za Ulaya, hatua inayoongeza matumaini kwa Dar City kufanya vizuri kwenye michuano hiyo ya bara.
Dar City itakuwa na kibarua kizito dhidi ya Johannesburg Giants, ambao pia ni wageni kwenye mashindano hayo lakini wameonesha kasi kubwa ya maendeleo tangu mwaka jana.
Akizungumza kutoka Afrika Kusini, Balozi wa Dar City, ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini, Revocatus Chipando ‘Baba Levo’, amesema timu hiyo imejiandaa kikamilifu na ipo tayari kwa mapambano.
“Tumejipanga vizuri, morali ya wachezaji ipo juu na kila mmoja anaelewa umuhimu wa kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania. Tuko tayari kupambana,” amesema Baba Levo.
Dar City inaingia kwenye BAL ikiwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri na kuandika historia mpya kwa mpira wa kikapu wa Tanzania kwenye jukwaa la Afrika.



