Kwingineko

Liverpool watinga robo fainali kibabe

LONDON, England KLABU ya Liverpool imefuzu hatua ya robo fainali ya UEFA Champions league baada ya kuichapa Galatasaray mabao 4-0 , ambapo sasa itakutana na mabingwa watetezi Paris St-Germain.

Baada ya kufungwa 1-0 katika mchezo wa kwanza uliochezwa Istanbul, kikosi cha kocha Arne Slot kilirejea kwa nguvu na kusawazisha jumla ya mabao kupitia kiungo Dominik Szoboszlai aliyefunga bao la kwanza kufuatia mpira wa adhabu uliopangwa vizuri.

Kabla ya mapumziko, mshambuliaji Mohamed Salah alikosa nafasi ya kuongeza bao baada ya penalti yake kuokolewa na kipa Ugurcan Cakir.

Hata hivyo, kipindi cha pili Liverpool waligeuka moto wa kuotea mbali kwa kufunga mabao matatu ndani ya dakika 11. Hugo Ekitike alifunga kwa karibu akimalizia pasi safi kutoka kwa Salah, kabla ya Ryan Gravenberch kufunga bao la tatu baada ya shuti la Salah kuokolewa.

Mlinzi Wilfried Singo aliujaza mpira wavuni kimakosa, lakini bao hilo lilikataliwa kutokana na Jeremie Frimpong kuwa ameotea. Dakika chache baadaye, Salah alipiga bao la kuvutia kwa shuti kali la nje ya boksi lililojaa kona ya juu.

Kwa bao hilo, Salah aliweka historia kwa kuwa mchezaji wa kwanza kutoka Afrika kufikisha mabao 50 katika UEFA Champions League.

Ushindi huo unamaanisha timu mbili za England zimefuzu robo fainali, huku Manchester City, Chelsea, Newcastle na Tottenham zikiaga mashindano hayo.

Related Articles

Back to top button