
WASHINGTON DC: Mchekeshaji maarufu duniani Kevin Hart ameibua mjadala mkubwa mitandaoni baada ya kushangazwa na sanamu yake ya wax iliyowekwa kwenye makumbusho nchini Marekani.
Kupitia video aliyochapisha, Hart aliikosoa sanamu hiyo akidai haifanani naye, kauli iliyosababisha mashabiki na mastaa wengine kuingia kwenye mjadala huo kwa utani na vichekesho.
Kevin Hart aliichapisha video hiyo akionesha sanamu hiyo huku akiikosoa vikali kwa kusema haifanani naye hata kidogo. Katika kauli yake ya utani lakini yenye msisitizo, alidai kuwa sanamu hiyo ni kama ‘shambulio’ dhidi yake na akaomba ifanyiwe marekebisho haraka.
Sanamu hiyo ipo katika makumbusho ya Hollywood Wax Museum, ambapo mastaa wengi huenziwa kwa kutengenezewa sanamu zinazofanana nao. Hata hivyo, kwa upande wa Hart, mashabiki wengi wamekubaliana naye kuwa haijafanikiwa kufanana naye ipasavyo.
Tukio hilo limezua vichekesho vingi mtandaoni, huku baadhi ya mastaa akiwemo Dwayne Johnson akitoa maoni yake kwa utani, akisema sanamu hiyo ni kamilifu jambo lililoongeza mzaha zaidi kwenye mjadala huo.
Mashabiki pia wamejitokeza kwa wingi wakitoa maoni yao, baadhi wakicheka na wengine wakitoa mapendekezo ya kuboreshwa kwa sanamu hiyo ili ifanane zaidi na muonekano halisi wa msanii huyo.




