La Liga
Frenkie De Jong nje wiki 6

BARCELONA:KLABU ya BARCELONA wamepata pigo zito baada ya Frenkie de Jong kupata majeraha yatakayomuweka nje kwa takribani wiki tano hadi sita. Kiungo huyo wa miaka 28 alilazimika kusitisha mazoezi baada ya kuhisi maumivu makali, na vipimo vya kitabibu vimeonesha kuwa ameumia misuli ya nyuma ya paja la mguu wa kulia.
Katika taarifa rasmi, klabu imethibitisha kuwa De Jong alipata majeraha kwenye sehemu ya misuli yake ya mguu wa kulia na muda wa kupona unatarajiwa kuwa kati ya wiki tano hadi sita. Hii ni habari mbaya kwa kocha Hansi Flick hasa kipindi hiki ambacho timu inaingia hatua muhimu za mashindano ya ndani na Ulaya.
Kabla ya majeraha haya, De Jong alikuwa ameanza kurejea kwenye kiwango chake bora. Alifunga bao lake la kwanza la msimu katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Levante, na eneo la kiungo la Barcelona lilikuwa limeanza kuonekana kuwa na uwiano mzuri hasa baada ya kurejea kwa Pedri.
Kwa miezi ya nyuma, De Jong alikuwa akibeba jukumu kubwa la ulinzi na ubunifu, mara nyingi akicheza kama kiungo wa chini peke yake huku akisaidiwa na Fermín López na Dani Olmo. Uwepo wa vijana kama Marc Bernal ulimpa nafasi ya kusogea mbele zaidi, eneo linaloendana na uwezo wake wa kukimbia na kubeba mpira.
Sasa, Flick atalazimika kupanga upya safu ya kiungo wakati timu ilikuwa imeanza kupata muonekano mzuri na utambulisho wa wazi uwanjani. Kipindi hiki ni cha maamuzi, na kukosekana kwa De Jong ni pigo linalokuja wakati mbaya zaidi.




