Familia

Lulu na Majizzo watimiza miaka mitano ya ndoa

Aahidiwa zawadi ya Private Jet!

DAR ES SALAAM: MREMBO wa filamu za Bongo, Elizabeth Michael maarufu kama Lulu, amesherehekea kwa furaha kubwa miaka mitano ya ndoa yake na mumewe kipenzi, Francis Siza ‘Majizzo’, wakiwa tayari wamebarikiwa watoto wawili.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Lulu alifunguka kwa hisia kali akimshukuru Mungu kwa kuwavusha salama katika safari ya ndoa yao na kuomba waendelee kushuhudia miaka mingine mingi zaidi.

“Kwa Neema ya Mungu tukaone mitano tena na zaidi. Ba’Mpenzi, Ba’mtu, Winga wa moyo wangu umepita bila kupingwa Baba,” aliandika Lulu kwa mahaba mazito.

Katika ujumbe huo uliogusa mioyo ya wengi, Lulu alimpongeza mumewe kwa uongozi wake thabiti ndani ya ndoa yao huku akitania kwa kusema licha ya “kubadilishwa kwa kreti za bia na mikungu ya ndizi” na makabila ya Wachaga na Wahaya, bado hajawahi kumuangusha kama kiongozi wa familia.

Muigizaji huyo aliendelea kumshukuru Majizzo kwa kumpenda, kumlea na kumtunza, akiongeza kwa utani kuwa anaendelea kuwa “mdogo mdogo kama Mandonga”.

Lakini kilichovuta hisia za wengi zaidi ni pale Lulu alipotaja mpango mzito unaokuja:
“Sasa kuna mchongo nausikilizia, mambo yakienda sawa… nakuchapa na Private Jet mtoto wa Ma’mkwe… si unanijua kuhusu malavidavi hii level chafu bebi.”

Kauli hiyo imeibua gumzo mitandaoni, mashabiki wakisubiri kuona kama kweli zawadi hiyo ya kifahari itatimia.

Amehitimisha, Lulu amemkabidhi tena “muhula mwingine” wa moyo wake kwa mumewe, akisisitiza kuwa anafurahia sana kuishi maisha yake pamoja naye.

“Happy 5th Anniversary Mumewangu… kama Moyo ni nchi nakukabidhi kwa muhula mwingine. Nakupentaaaa,” amemaliza Lulu kwa mahaba tele.

Maadhimisho hayo yanaonyesha namna wawili hao wameendelea kujenga ndoa yao kwa upendo, furaha na utani wa kimahaba, wakithibitisha kuwa penzi lao linaendelea kushika kasi hata baada ya miaka mitano kupita.

Related Articles

Back to top button