Wahalifu wavunja na kuiba ghala la rapa Central Cee

LONDON: RAPA maarufu wa Uingereza Oakley Caesar-Su maarufu Central Cee, ameripotiwa kupoteza mali ya thamani kubwa baada ya wahalifu kuvamia ghala lake la kuhifadhia mizigo na kuiba sehemu kubwa ya mkusanyiko wake wa viatu (sneakers) aliokuwa amekusanya kwa zaidi ya miaka 12.
Msanii huyo mwenye umri wa miaka 27 alithibitisha tukio hilo kupitia ukurasa wake wa Instagram, ambapo alichapisha picha zinazoonesha hali halisi baada ya uvamizi huo, yakiwemo maboksi tupu za viatu yakiwa zimetapakaa sakafuni.
Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na Yahoo News, Central Cee alieleza kuwa mkusanyiko huo ulijengwa kwa zaidi ya muongo mmoja, jambo linalofanya hasara hiyo kuwa si tu ya kifedha bali pia ya kihisia.
“Ghala langu la viatu liliibiwa siku chache zilizopita,” aliandika rapa huyo, akiwakumbusha mashabiki wake kuwa viatu hivyo alivikusanya kwa miaka mingi
Central Cee pia alisema miongoni mwa vilivyoibwa kulikuwa na jozi yenye thamani ya kipekee kwake, iliyohusishwa na hatua za mwanzo za safari yake ya muziki.
“Ndani kulikuwa na Nike ID Air Force 1 yangu ya kwanza niliyonunua Alboraaq mwaka 2015,” aliandika, akiambatanisha ujumbe huo na alama ya huzuni.
Ufunuo huo uliibua hisia tofauti mtandaoni. Wakati wengi walimtumia jumbe za pole na kumuonesha huruma, baadhi ya mashabiki walihoji muda wa tangazo hilo, hasa likizingatiwa kuwa limekuja wakati rapa huyo ameanza kampeni ya kutangaza ushirikiano mpya wa biashara ya viatu.
Licha ya changamoto hiyo, msanii huyo aliwahimiza mashabiki wake kuunga mkono mradi huo mpya.
“Lakini kila kitu kimeandikwa, hata hivyo, nunueni kiatu changu kitakapotoka,” aliandika.
Mbali na tukio hilo la wizi, Central Cee anaendelea kufurahia mafanikio makubwa katika tasnia ya muziki. Mwaka 2025 aliandika historia katika tuzo za MOBO baada ya kushinda kipengele cha Msanii Bora wa Kiume (Best Male Act), akifikisha jumla ya tuzo saba sawa na rapa Stormzy.
Pia ameteuliwa katika vipengele vya Msanii Bora wa Kiume na Albamu Bora kwa kazi yake Can’t Rush Greatness, huku hafla ya utoaji tuzo ikitarajiwa kufanyika mwezi Machi.



