
DAR ES SALAAM:MWIMBAJI wa nyimbo za Injili nchini Tanzania, Miriam Mauki, amesema kuwa mara nyingi kile ambacho binadamu hukiona kama hapana kutoka kwa Mungu, huwa ndicho jibu sahihi na salama kwa wakati husika.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Mauki aliwaasa waumini na mashabiki wake kumruhusu Mungu abaki kuwa Mungu, hata pale ambapo majibu yao ya maombi hayaji kwa namna wanayotamani.
“Ila huyu Mungu mwacheni abaki kuwa Mungu. Hata kama kuna vitu hajakujibu kwa namna ulivyotamani vijibiwe, wewe mwache abaki kuwa Mungu kwako, usimpunguze,” ameandika.
Ameongeza kuwa hapana ya Mungu huwa ni jibu kamili kwa wakati husika, hata kama linaumiza au halieleweki mara moja.
“Kwa kuwa hapana yake ndicho kilikuwa jibu lako kwa wakati huo,” amesisitiza.
Akisimulia uzoefu wake binafsi kabla ya ndoa, Mauki alisema aliwahi kuwa kwenye mahusiano ambayo Mungu aliyafunga, jambo lililomsababishia maumivu ya nafsi kwa kipindi fulani, bila kujua kuwa ilikuwa ni njia ya Mungu kumlinda.
“Kuna wakati kabla ya ndoa nilikuwa kwenye mahusiano fulani, halafu Mungu akaufunga ule mlango wa mahusiano yale. Nafsi yangu ilianza kupata shida, lakini kumbe lilikuwa jibu la usalama wa hatima yangu,” amesema.
Kutokana na hilo, aliwahimiza watu wasiogope hapana ya Mungu kwani hubeba majibu ya usalama wao.
“Usiogope ‘No’ ya Mungu, ni jibu la salama yako,” ameandika.
Katika ujumbe wake, Mauki pia alizungumza kuhusu mahusiano, akieleza kuwa si kila uhusiano huenda mpaka kwenye ndoa, na hilo ni jambo la kawaida.
“Kuna wale wanatamani mahusiano wanayoanza yawe ndiyo hayo mpaka ndoa, mmmmm si kweli. Inawezekana ikawa hivyo au isiwe,” amesema.
Alifafanua kuwa ndiyo maana huitwa mahusiano na si ndoa, kwa kuwa ni hatua ya kuangaliana na kutambua kama wahusika wanaweza kufika kwenye ndoa.
Hata hivyo, aliwashauri wale wanaoona mahusiano yao hayaleti taswira ya maisha ya baadaye wanayoomba na kuiota, wasisite kuchukua uamuzi wa kujitoa.
“Kama umeanza kuyaona hayaleti sura ya kesho unayo iota na kuiombea, usisite kushuka kwenye hiyo safari,” alihitimisha.




