Nyumbani

Yanga warejea mazoezini, macho yote kimataifa

DAR ES SALAAM: KLABU ya Yanga SC imerejea mazoezini leo kuanza maandalizi ya awamu ya kwanza, ambapo itafanya mazoezi kwa wiki moja kabla ya kuingia mapumziko mafupi.

Baada ya hapo, kikosi hicho kinatarajiwa kurejea tena kambini tarehe 29, mara baada ya wachezaji wote waliokuwa na majukumu mbalimbali kurejea, ili kuingia kwenye maandalizi mazito zaidi.

Kwa mujibu wa Msemaji wa Yanga, Ally Kamwe, maandalizi hayo yanalenga mashindano mawili makubwa yanayoikabili timu hiyo, ambayo ni Ligi Kuu ya NBC pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kamwe amesema benchi la ufundi linajipanga kuhakikisha kikosi kinakuwa katika hali bora ya ushindani kabla ya kurejea kwenye ratiba ngumu ya mashindano ya ndani na kimataifa.

Yanga inajiandaa pia kwa mchezo mkubwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri, ambapo mchezo wa mkondo wa kwanza unatarajiwa kuchezwa kati ya Januari 23, kabla ya mchezo wa marudiano Januari 30.

Katika hatua nyingine, Yanga imetajwa kuwa miongoni mwa timu zinazotarajiwa kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi itakayofanyika Zanzibar, ingawa uongozi wa klabu hiyo bado haujaweka wazi msimamo rasmi kuhusu ushiriki wao.

Michuano hiyo inatarajiwa kuanza Desemba 28 hadi Januari 13, na kushirikisha timu mbalimbali za ndani na nje ya nchi.

Kwa ujumla, kurejea kambini kwa Yanga ni ishara ya maandalizi makini kuelekea kipindi kigumu cha msimu, huku mashabiki wakingoja kuona hatima ya ushiriki wao Kombe la Mapinduzi pamoja na maandalizi yatakayowawezesha kuhimili presha ya michezo ya ndani na Afrika.

Related Articles

Back to top button