Tetesi

George Mpole ajiweka sokoni

DAR ES SALAAM: ALIYEKUWA mshambuliaji wa FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Mtanzania, George Mpole amesema bado hajasaini timu yoyote, licha ya kupokea ofa nyingi kutoka klabu mbalimbali ndani na nje ya Tanzania.

Kuna taarifa kuwa mshambuliaji huyo amemalizana na uongozi wa Yanga kwa kusaini mkataba wa miaka miwili kutumikia timu hiyo kwa msimu wa 2024\25.

Spotileo lilimtafuta Mpole ambaye amesema mkataba wake na FC Lupopo umemalizika, na tayari amepokea ofa nyingi kwa ndani ikiwemo Yanga na timu zingine lakini pia kutoka nje ya nchi.

Amesema bado hajasaini Yanga licha ya kuwepo kwa mazungumzo na uongozi wa klabu hiyo kuangalia jinsi gani ya kwenda kuongeza nguvu ndani ya kikosi cha mabingwa hao wa kihistoria.

“Mimi ni mchezaji huru baada ya mkataba wangu na Lupopo kufikia tamati, ofa zipo nyingi siwezi kuzitaja zote hizo, hiyo Yanga, Simba nipo nao kwenye mazungumzo na kikubwa naangalia kwenye ofa ambayo nimeitaka,” amesema Mpole.

Ameongeza kuwa bado hajafikiana na klabu yoyote kati ya hizo kwa sababu mazungumzo yanaendelea, anaangalia maslahi pamoja na nafasi ya kwenda kucheza.

Mpole aliwahi kuwa mfungaji bora wa msimu wa 2020\21 wa Ligi Kuu Bara akiwa jumla ya mabao 17 na pasi 4 za mabao wakati anacheza Geita Gold FC ambayo imeshuka daraja, huku akifuatiwa na mshambuliji wa Yanga, Fiston Mayele aliyemaliza msimu akiwa na mabao 16 na pasi 5 za mabao.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button