
DAR ES SALAAM: SINGIDA Black Stars imeahidi kufanya maboresho katika kipindi cha mapumziko ya kalenda ya FIFA ili kurejesha makali yake baada ya mwenendo wa kusuasua katika michezo kadhaa iliyopita ya Ligi Kuu.
Katika michezo mitano iliyopita ya ligi, Singida imeshinda mchezo mmoja pekee, ikipata sare moja na kupoteza michezo mitatu matokeo yaliyozidi kuwashusha kutoka nafasi za juu hadi ya tisa kwa pointi 14 kwa jumla ya michezo 10.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Singida Black Stars Hussein Masanza amesema mapumziko hayo ni fursa kwa benchi la ufundi chini ya kocha Papic Kimoto kufanyia kazi maeneo yenye changamoto, huku akieleza kuwa kupoteza alama katika michezo mbalimbali, ikiwemo dhidi ya Mbeya City jijini Mbeya, si matokeo yanayokidhi matarajio yao.
Amesema mwenendo huo si taswira halisi ya Singida Black Stars waliyoizoea wadau na mashabiki, hivyo benchi la ufundi na wachezaji wameanza kuchukua hatua kuhakikisha timu inarejea katika ubora wake.
“Tunafahamu mwenendo wa timu yetu upande wa ligi umekuwa kidogo wa kusuasua. Tunapoteza alama hata katika mchezo tuliocheza dhidi ya Mbeya City kule Mbeya, ambapo tulidondosha alama zote tatu.
“Hii si Singida Black Stars ambayo imezoeleka na hilo ndilo tunalolifanyia kazi kwa kiasi kikubwa katika kipindi hiki cha mapumziko mafupi,” amesema.
Hata hivyo, amewatoa hofu mashabiki na wadau wa timu hiyo, akisisitiza kuwa bado wana imani na hesabu zao katika ligi, huku akiahidi kuwa maboresho yanayofanywa yataifanya timu kurejea ikiwa imara zaidi.
Amesema lengo lao la kumaliza katika nafasi nne za juu na kupata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao bado lipo pale pale.
Katika hatua nyingine, Masanza amesema klabu hiyo imetuma barua ya maombi ya kutaka kutumia Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam kwa ajili ya kucheza mechi zake za nyumbani katika hatua ya makundi ya michuano ya kimataifa.
Amesema hatua hiyo imekuja kufuatia klabu hiyo kufanikiwa kufuzu hatua ya makundi.




