Wastara Juma: Ndoto yangu ni kununuliwa hata pikipiki

DAR ES SALAAM: MWIGIZAJI wa filamu nchini, Wastara Juma, amesema kuwa katika maisha yake ya kimahusiano hajabahatika kupata zawadi kubwa kutoka kwa wanaume aliowahi kuwa nao, akifichua kuwa moja ya ndoto zake ambazo hazijawahi kutimia ni kununuliwa pikipiki.
Wastara amesema kuwa tofauti na baadhi ya wanawake ambao wamekuwa wakipokea zawadi za magari ya gharama kubwa, nyumba na vitu vingine vya thamani kutoka kwa wenzi wao, yeye bado hajapata bahati hiyo, hata katika zawadi ambayo kwake inaonekana kuwa ya kawaida kama pikipiki.
Akizungumzia suala hilo, mwigizaji huyo ameeleza kuwa wapo wanawake waliobahatika kuwa na wanaume wanaojua wajibu wao katika mahusiano na ndoa, hivyo kuwajali kwa kuwapatia mahitaji na zawadi mbalimbali.
Hata hivyo, Wastara amedai kuwa kupokea zawadi kubwa kutoka kwa mwenzi wako si lazima kuwe ishara ya uaminifu katika mahusiano, akieleza kuwa baadhi ya wanaume wanaowahudumia vizuri wenzi wao bado wanaweza kuwa na mahusiano mengine ya pembeni.
Ametoa mfano wa rafiki yake aliyewahi kumuonesha zawadi mbalimbali alizokuwa akipewa na mwenzi wake, lakini wakati huohuo akamweleza kuwa mwanaume huyo alikuwa na uhusiano mwingine nje ya mahusiano yao.
Kwa mtazamo wake, bahati katika maisha ya mahusiano hutofautiana kati ya mtu na mtu, huku akisisitiza kuwa wale waliojaaliwa kupata wenzi wanaowajali na kuwathamini wanapaswa kuitunza bahati hiyo.
Wastara ameeleza kuwa wakati mwingine bahati ya mtu inaweza kumletea mambo mazuri licha ya makosa aliyowahi kufanya, akisisitiza kuwa kuna watu wanaobahatika kupata vitu vizuri katika maisha yao ya kimahusiano.




