AFCON

2024 ilikuwa ya Taifa Stars

MWAKA 2024 utakumbukwa mno na Watanzania baada ya timu ya taifa Taifa Stars kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa mara ya nne katika historia. Taifa Stars iliyotoka kushiriki fainali za mwaka 2023 zilizofanyika mwaka 2024 nchini Ivory Coast ililazimika kusubiri hadi mchezo wa mwisho ili kujihakikishia tiketi ya kwenda kushiriki michuano hiyo nchini Morocco.

Katika kampeni ya kufuzu Taifa Stars ilikuwa kundi H Pamoja na timu za DR Congo, Guinea,na vibonde wa kundi hilo Ethiopia. Stars ilimaliza katika nafasi ya pili ambapo ilishinda michezo mitatu, sare moja na kupoteza michezo miwili wakivuna jumla ya alama 10 alama nyingi zaidi kuwahi kuvuna katika kampeni ya kufuzu mashindano ya AFCON.

Vita ya kuisaka tiketi hiyo ilikuwa kali baina ya Taifa Stars na Guinea ambapo ilivyokuwa bahati timu hizo zilipaswa kukutana uso kwa uso na mshindi angeipata nafasi ya kufuzu michuano hiyo ya Morocco. Mchezo huo ulipigwa katika Uwanja wa Benjamini Mkapa Novemba 19, 2024 na Taifa Stars kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Katika siku hiyo Watanzania walijitokeza kwa wingi katika dimba la Benjamini Mkapa ambapo Rais Samia Suluhu Hassan alinunua tiketi kwa mashabiki kwenda kuishangailia timu yao na dhamira ya kuufanya uwanja huo kuwa tanuru la moto kwa wapinzani ilitimia baada ya uwanja kutapika Watanzania na kuchagiza ushindi huo huku shujaa akiwa Simon Msuva aliyekwamisha mpira wavuni dakika ya 60.

Hii ni mara ya nne Taifa Stars kufuzu Afcon baada ya kushiriki Makala ya mwaka 1980, 2019, 2023 iliyofanyika 2024 na sasa wanatamba na tiketi ya kushiriki michuano ya mwaka 2025 huko Kaskazini mwa Afrika.

Shauku ya Watanzania ni kuona muendelezo wa Taifa Stars katika ushiriki wake kwenye michuano hiyo baada ya kupata alama mbili kwenye michuano iliyopita nchini Ivory Coast ambapo ni nyingi zaidi katika mara zote walizoshiriki je mwaka 2025 itakuaje? Tukutane Morocco.

 

Related Articles

Back to top button