Filamu

Wasanii kupatiwa mafunzo ya siku 5

Wasanii wa tasnia mbalimbali za sanaa waitwa kupatiwa mafunzo yatakayowasaidia kuendeshea kazi zao katika Tamasha la Kimataifa la Maendeleo ya Filamu na Sanaa Tanzania lililoandaliwa na Bodi ya Filamu Tanzania ambalo limeanza kufanyika leo Desemba 11 hadi 15 katika viwanja vya Posta Kijitonyama jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia tamasha hilo Kaimu Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Filamu nchini Gervas Kasiga amesema Tamasha hilo linatarajiwa kuzinduliwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, utamaduni, Sanaa na Michezo Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’

“Nipende kuchukua nafasi hii kuwakaribisha wasanii mbalimbali kuja kushiriki katika tamasha litakaloleta mabadiliko katika sekta ya filamu kutokana na mafunzo na midahalo mbalimbali itakayosaidia wasanii kukua katika Sanaa yao.

“Sio kwa wasanii wa filamu peke yao, bali hata wasanii wa bongo fleva na sanaa mbalimbali wajitokeze na kujifunza kwa yanayofundishwa katika tamasha hili ikiwa ni kufanya kazi bora za sanaa kuangalia masoko na kutangaza kazi kitaifa na kimataifa. Tutakuwepo kwa muda wa siku tano katika viwanja vya Kijitonyama.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Cosota Doreen Sinare amesema kuwa
wataendelea kutoa elimu kwa wasanii jinsi ya kujisajili na kusajili kazi zao ili kukuza na kulinda kazi zao.

“Bado wasanii wanapitia changamoto kwenye mikataba yao na sisi tutaendelea kuwapa elimu ili waweze kuingia mikataba mizuri itakayowasaidia wao na vizazi vyao sio itakayowafunga maisha” amesema Doreen Sinare.

Related Articles

Back to top button