Zaylissa humbuambii kitu kwenye stara

DAR ES SALAAM:MUIGIZAJI wa filamu za Bongo, ambaye ni bibi harusi Zaylissa Said, amezua mjadala mzito mitandaoni baada ya kuzungumzia suala la uvaaji wa stara na namna unavyoweza kumpendezesha mtu kuliko mavazi ya kuacha maungo wazi.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Zaylissa alishiriki picha akiwa amevalia mavazi ya heshima na kuambatanisha ujumbe uliowavutia wengi.
“Hivi nani alikwambia stara haimpendezi mtu???? Na sio kupendeza tu! Unavaa nguo zipi????” ameandika Zaylissa.
Kauli hiyo imeibua gumzo miongoni mwa mashabiki wake, wengi wakionesha kuunga mkono msimamo wake kwamba kujisitiri ni alama ya heshima na thamani binafsi.
Zaylissa amesisitiza kuwa urembo wa kweli haupatikani kwa kuanika maungo ya mwili, bali katika namna mtu anavyojiheshimu na kujisitiri. Kwa mujibu wa muigizaji huyo, kuvaa mavazi ya stara kunaongeza mvuto wa kipekee na kuonesha ukomavu wa fikra.
Kauli yake imefungua mjadala mpana kuhusu mitindo ya mavazi katika jamii ya sasa, hususan kwa vijana na wasanii, huku baadhi wakieleza kuwa kila mtu ana uhuru wa kuchagua anachovaa, ilhali wengine wakisisitiza umuhimu wa maadili na heshima.




