Yanga kuifuata Al Hilal Okt 15 alfajiri

MSAFARA wa wachezaji 25 wa timu ya Yanga, unaondoka Oktoba 15 alfajiri kwenda Sudan kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa kufuzu hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal.
Akizungumza na Spotileo Kocha Mkuu wa timu hiyo Nasreddine Nabi amesema timu hiyo itafanya mazoezi ya mwisho Oktoba 14 jioni kambini Avic Town iliyopo Kigamboni, Dar es Salaam.
Amesema wachezaji wote wapo tayari kwa safari hivyo kazi inabaki kwake kuchagua ni mchezaji gani amwanzishe kwenye mchezo huo ambao ushindi ni kipaumbele namba moja.
“Taarifa ya madaktari ambayo nimeipokea mchana huu imenifurahisha inasema wachezaji wangu wote wapo sawa kiafya kitu ambacho kina nipa matumaini ya kufanya vizuri kwenye mchezo wetu wa Jumapili huko Sudan,” amesema Nabi.

Yanga itashuka dimbani Oktoba 16 katika wa uwanja wa Al- Hilal uliopo mji wa Omdurman katika Jimbo la Khartoum, Sudan kumenyana na wenyeji wao Al Hilal huku ikihitaji ushindi au sare ya kuanzia mabao 2-2 ili kucheza hatua ya makundi.
Katika mchezo wa kwanza uliopigwa katika uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.