Africa

Aweso ashusha tamko Simba

DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Maji, Juma Aweso, ameungana na Watanzania wengine kuipongeza klabu ya Simba  baada ya kuvunja mwiko na kutinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, mafanikio yaliyosubiriwa kwa muda mrefu.

Katika mchezo wa kuvutia uliopigwa dhidi ya Al Masry, Simba walifanikiwa kusawazisha matokeo ya jumla kwa ushindi wa mabao 2-0 katika dakika 90 za kawaida, kabla ya kuhitaji mikwaju ya penalti ambapo walishinda kwa 4-1 na kufuzu hatua ya nusu fainali.

Akizungumza baada ya ushindi huo, Waziri Aweso alisisitiza kuwa ushindi huo ni matokeo ya jitihada na mshikamano wa wachezaji pamoja na benchi la ufundi.

“Niwapongeze wote  wachezaji, benchi la ufundi, na mashabiki. Bahari kubwa huvukwa kwa juhudi na kwa kweli tumevuka kwa kishindo. Kilichopo mbele yetu sasa ni kulitaka kombe hili, na tunaweza kulipata,” amesema Aweso kwa matumaini makubwa.

Simba sasa wanajiandaa kuvaana na Stellenbosch ya Afrika Kusini katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali unaotarajiwa kuchezwa Aprili 20. Stellenbosch wao walitinga hatua hiyo baada ya kuifunga Zamalek kwa bao moja pekee.
Hii ni mara ya kwanza kwa Simba kufika hatua ya nusu fainali ya michuano ya CAF tangu mwaka 2021 walipofika hatua kama hiyo katika Kombe la Shirikisho. Aidha, kumbukumbu ya mbali zaidi ni mwaka 1993 walipofika nusu fainali ya CAF Cup – wakati huo ikijulikana kwa jina hilo.

Katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba wamewahi kufika hatua ya robo fainali mara kadhaa, ikiwemo mwaka 2021 walipoondolewa na Kaizer Chiefs kwa faida ya mabao ya ugenini.

Safari yao sasa ni ya kihistoria na kila mshabiki soka nchini anasubiri kwa hamu kuona kama hatimaye Simba wataweza kuweka historia mpya kwa kutwaa taji la Afrika.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button