Africa

YANGA bado ina nafasi kutinga makundi

KUKATA tamaa katika jambo lolote lile ni dhambi kubwa katika maisha ya mwanadamu eliyekuwa hai, ipo aya kwenye Quraan tukufu inakemea mtu kupoteza matumaini kutokana na ugumu au magumu anayopitia kwa kipindi hicho.

Sio tu kwa Waislamu hata kwa Wakristo pia inaelezwa kuwa kukata tamaa ni dhambi kubwa.

Kitendo cha Yanga kutoa suluhu dhidi ya Club Africain ya Tunisia, Jumatano iliyopita kimewakatisha wengi tamaa, ikiwemo wanachama na mashabiki wao wakiamini timu hiyo tayari imeondoshwa katika harakati za kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.

Katika hilo hakuna ukweli Yanga inayo nafasi kubwa ya kusonga mbele hatua ya makundi kuliko wapinzani wao Club Africain licha ya kwamba wameshindwa kupata ushindi uwanja wa nyumbani.

Kinachoipa nafasi hiyo Yanga ni aina ya matokeo waliyoyapata ya suluhu hii inatoa presha kwa timu zote mbili, hasa aliyekuwa nyumbani sababu atakuwa akicheza kwa presha kubwa kuhakikisha mpinzani hapati bao.

Sababu ikitokea Yanga anapata bao moja itakuwa wamewapa mlima mrefu Club Africain kuhakikisha wanafunga bao zaidi ya moja ili kutinga hatua ya makundi ambayo ndiyo lengo la uongozi wachezaji na mashabiki wa timu hiyo.

Kitu cha msingi kwa Yanga, wanapaswa kurudisha hali ya kujiamini na kwenda kupambana kutafuta matokeo na siyo kwenye kupaki basi na kuruhusu mashambulizi kwenye lango lao jambo hilo linaweza kuwarahisishia kazi Club Africain.

Wachezaji wa Yanga, hawapaswi kuingia uwanjani vichwani mwao wakifikiria matokeo ya mchezo uliopita au endapo ikitokea wametolewa watawaeleza nini mashabiki wao.

Kitu cha msingi wanatakiwa kujiamini na kujiona hawapo hapo kwa bahati mbaya bali ni uwezo wao ndio umesababisha Injinia Hersi na jopo lake kutoa gharama kubwa za pesa kuwasajili.

Yanga wanatakiwa kujua pamoja na fitna zilizopo kwenye michuano hiyo hasa kwa timu iliyo nyumbani lakini kizuri hakijifichi, walikwenda Sudan kucheza na Al Hilal na wakafungwa, lakini pamoja na vurugu za mashabiki wa timu hiyo baada ya mpira waliwapigia makofi Yanga kutokana na soka safi walilo lionesha.

Ukatili huo wanaweza kuuhamishia Tunisia wakacheza soka lao la kila siku na kupata matoke bila kujali kwamba timu zinazotokea Kaskazini zimekuwa zikitumia hila nyingi kwa ajili ya kutaka ushindi.

Mchezo wa soka unachezwa hadharani kila mtu anaona sidhani kama kuna ulazima Yanga kuingiwa na baridi na kujikatia tamaa wakati mpaka sasa nafasi ya kucheza hatua ya makundi bado ipo mikononi mwao.

Ipo mifano mingi ambayo inaifanya Yanga isijione wanyonge kwa kushindwa kupata ushindi mfano mwaka 2002 Yanga ilishiriki michuano hiyo na ilipangiwa kuanza nyumbani Uwanja wa Taifa ambao sasa Uhuru dhidi ya Highlanders FC ya Zimbabwe.

Katika mchezo wa kwanza timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2 na baada ya mchezo kumalizika kocha wa Highlanders akisema kama angekuwa yeye kocha wa Yanga asingepeleka timu Zimbabwe.

Lakini kitu cha kushangaza baada ya Yanga kwenda Zimbabwe hadi mapumziko Yanga walikuwa wanaongoza kwa mabao 2-0 na kipindi cha pili Yanga wakapata mkwaju wa penalti wenyeji Highlanders wakaanzisha vurugu na kugomea mchezo.

Baadaye Caf , waliipa adhabu Highlanders na kuipeleka Yanga hatua inayofuata, lakini mfano mwingine uliokuwa hai ni katika michuano hii ambayo inaendelea hivi sasa, Vipers ya Uganda imewatoa T.P Mazembe.

Katika mchezo wa kwanza uliopigwa Uganda timu hizo zilitoka suluhu, lakini Vipers hawakukata tamaa walikwenda Lubumbashi wakiwa wanajiamini na walikwenda kupambana na kufanikiwa kuiondosha miamba hiyo ya Afrika bila kutarajiwa.

Club Africain tumewaona siyo timu ya kutisha sana, hivyo hakuna lisilowezekana.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button