Xouh amkumbusha Nandy mchango wa Ruge:

DAR ES SALAAM: MSANII wa muziki wa Bongo Fleva, Xouh, amemkumbusha msanii mwenzake Nandy kuhusu mchango wa marehemu Ruge Mutahaba katika safari yake ya muziki, akisisitiza kuwa mchango wake haupaswi kutazamwa kwa mtazamo wa kuwa chini ya lebo pekee.
Kauli hiyo ya Xouh imekuja kufuatia maelezo ya Nandy kuwa hajawahi kuwa chini ya lebo yoyote ya muziki, jambo lililomfanya Xouh kuibua mjadala kuhusu tofauti kati ya kuwa chini ya lebo na kupata usimamizi, mwongozo na uwekezaji kutoka kwa wadau wa muziki.
Akieleza hisia zake, Xouh amesema imemuuma kusikia kauli hiyo kwa sababu, kwa mtazamo wake, Ruge alifanya kazi kubwa zaidi ya majukumu ya kawaida ya lebo kwa kusaidia, kulea na kuendeleza vipaji vya wasanii nchini.
“Imeniuma sana kusikia mtu akisema kwamba hajawahi kuwa kwenye label, akimaanisha kwamba hajawahi kusimamiwa, kusaidiwa au kuwa na mtu nyuma yake.
“Je, kutokuwa kwenye label ndiyo kusema umetoka kwa nguvu na akili zako mwenyewe?” amehoji Xouh.
Amesema marehemu Ruge alikuwa zaidi ya msimamizi wa lebo, kwani alitekeleza majukumu ya mshauri, mlezi na mentor kwa wasanii wengi, akiwasaidia kukuza vipaji na kujenga safari zao za muziki.
“Hivi mmemsahau marehemu Ruge? Mtu ambaye alifanya zaidi ya kazi za label. Alikuwa mentor, mshauri, mlezi na mtu aliyejenga vipaji vingi vya muziki wa Tanzania,” amesema.
Ameongeza kuwa kuna tofauti kati ya kuwa chini ya lebo na kuwa na mtu anayekuamini, anayekuongoza na kuwekeza katika kazi zako za muziki.
Katika hatua nyingine, Xouh ameeleza uzoefu wake binafsi, akisema alianza safari yake ya muziki bila kuwa na mtu wa kumsaidia kifedha, kumtafutia miunganisho au kumpa mwongozo wa namna ya kuendesha kazi yake.
“Mimi kama msanii, nilianza from scratch. Bila connection, bila mtu wa kunipa hata senti mia ya kuwekeza kwenye muziki wangu.
“Sikuwahi kuwa na mtu wa kunipa support ya kifedha, mawazo au mwongozo wa namna ya kuendesha career yangu,” amesema.
Amesema alilazimika kujifunza, kujipanga na kupambana mwenyewe hadi kufikia hatua ya kujenga nafasi yake katika tasnia ya muziki wa Tanzania.
“Nilijifunza, nilijipanga na nikapambana kwa nguvu zangu mwenyewe. Leo hii, ukitaja wasanii wa kike wanaofanya vizuri Tanzania, jina langu haliwezi kukosekana. Na hata ukilisahau, Watanzania watakukumbusha,” amesema Xouh.
Kauli hiyo imeibua mjadala kuhusu nafasi ya wasimamizi, walezi na wadau wengine katika kukuza vipaji vya wasanii, pamoja na umuhimu wa kutambua mchango wa watu waliochangia mafanikio ya muziki wa Tanzania.




