Kim Kardashian: Nilipoachana na Kanye nilikaa ‘singo’ miaka mitano

NEW YORK: SUPASTAA Kim Kardashian amefichua kuwa aliishi bila kuwa na mpenzi kwa takriban miaka mitano baada ya kutengana rasmi na baba watoto wake, rapa Kanye West.
Kim amefunguka lengo lake la kufanya hivyo ni kuweka kipaumbele kwa watoto wake na yeye mwenyewe na hiyo ilimpa hisia nzuri sana.
Mrembo huyo, 45 ameliambia gazeti la The Times kuwa hayo hayahusiani na kipindi kifupi cha mwaka huo alipokuwa na uhusiano na mwigizaji, Pete Davidson.
“Kwa kweli niliishi bila mpenzi kwa miaka mitano. Na hilo lilinipa hisia nzuri sana. Nilijikita kwa watoto wangu na miradi ambayo nilitaka kushiriki na sikuwa na haraka yoyote.”
Alifichua kuishi bila mpenzi hakukumfanya ajihisi mpweke na kwamba alihitaji zaidi muda wake mwenyewe.
“Nilitaka kupona kabisa na kujijenga mwenyewe. Sikuwa tayari kufungua mlango wa uhusiano mpya. Kwa kweli sikuwa hata nikiwaza kuhusu hilo. Mambo ya ulimwengu hufanya kazi kwa faida yako pale unapoyaruhusu tu yatiririke.”
Katika mahojiano hayo ya kina, Kim alikataa kuzungumzia uhusiano wake na mpenzi wake wa sasa, Lewis Hamilton, akisema: “Kwa heshima kubwa, ningependelea kutozungumzia hilo.”
Kim na Lewis, 41 ambaye ni dereva wa Formula One wanaonekana katika hali nzuri ya kimapenzi kwa muda sasa.
Wawili hao walionekana huko Aspen, Colorado, kwenye sherehe ya mkesha wa mwaka mpya ya Kate Hudson, kabla ya kuhudhuria fainali ya Super Bowl pamoja mwezi Februari.
Tangu wakati huo, wamekuwa wakichapisha picha zao pamoja mtandaoni mara kwa mara.




