
DAR ES SALAAM: KLABU ya kikapu ya UDSM Outsiders imeanza kwa kishindo Ligi ya Kikapu ya Mkoa wa Dar es Salaam, baada ya kushinda mechi tatu mfululizo na kujikusanyia pointi sita ambazo zimewaweka kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.
Outsiders walimaliza msimu uliopita wakiwa nafasi ya pili, baada ya kufungwa na JKT katika fainali. Msimu huu, wameanza kwa kasi kubwa ambapo tangu kuanza kwa ligi wiki mbili zilizopita, wamecheza michezo mitatu na kushinda yote huku wakifunga jumla ya pointi 207. Katika mchezo wao wa jana Jumapili, waliibuka na ushindi mnono wa pointi 78-42 dhidi ya Mgulani JKT.
Mabingwa watetezi JKT nao wameanza vyema, wakiwa nafasi ya pili kwa pointi tano baada ya kushinda michezo miwili kati ya mitatu. Stein Warriors waliopanda daraja msimu huu wameshika nafasi ya tatu wakiwa na pointi sawa na JKT, wakifuatiwa na Dar City ambao wako nafasi ya nne lakini wakiwa wamecheza michezo miwili pekee – jambo linalowapa nafasi ya kupanda nafasi kulingana na matokeo yajayo.
Matokeo ya michezo ya Jumapili yalikuwa: Stein Warriors 93-74 Savio, Dar City 105-32 Srelio, JKT 88-55 Polisi, DB Troncatti 67-47 Reel Dream, Vijana Queens 66-36 Kigamboni Queens, na Don Bosco Lioness 73-28 City Queens.