UDSM Outsiders, JKT kuchuana kesho
DAR ES SALAAM: FAINALI ya pili Ligi ya kikapu Mkoa wa Dar es Salaam kati ya UDSM Outsiders dhidi ya JKT Tanzania inatarajiwa kuchezwa kesho katika viwanja vya Don Bosco Osyterbay.
Timu hizo zilishindwa kuendelea na fainali hiyo awali, baada ya Chama cha Kikapu kutangaza kusimamisha kufuatia ujio wa Ligi ya taifa ya kikapu iliyofanyika Dodoma hivi karibuni ili kuzipa timu nafasi ya kushiriki.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Ufundi na Mashindano wa Chama cha Kikapu Dar es Salaam Haleluya Kavalambi, ligi hiyo imerejea na itaendelea kesho Jumamosi majira ya saa mbili usiku.
“Tunapenda kuwatangazia kuwa mchezo wa pili wa fainali ya wanaume ligi ya mkoa utachezwa Jumamosi,”ilisema taarifa ya Kavalambi.
Fainali ya kwanza JKT ilishinda kwa pointi 67-62 katika mchezo wa mwisho uliochezwa mwanzoni mwa mwezi Novemba mwaka huu.
Tayari mshindi wa tatu ni mabingwa wa mkoa msimu uliopita wa 2023 Dar City aliyeibuka mshindi dhidi ya Savio kwa pointi 72-51.