Trey Songz avutiwa na ngoma za asili

DAR ES SALAAM: Mkali wa muziki wa R&B kutoka Marekani, Trey Songz, ametua nchini Tanzania tayari kwa kushiriki Tamasha la CRDB IMBEJU Sauti Moja Concert litakalofanyika Agosti 14, 2026 katika Viwanja vya Posta Kijitonyama jijini Dar es Salaam.
Msanii huyo anayefahamika kupitia nyimbo mbalimbali zilizotikisa duniani, ikiwemo ‘Bottoms Up’, aliwasili usiku wa manane katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), ambapo alipokelewa na kupokelewa na msanii wa Bongo fleva Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’,mashabiki pamoja na waandaaji wa tamasha hilo.
Mara baada ya kuwasili, Trey Songz alionekana kuvutiwa na burudani ya ngoma za asili za Tanzania zilizotolewa kama sehemu ya mapokezi yake, jambo lililoonyesha kuguswa kwake na utamaduni wa nchi.
Trey Songz ni miongoni mwa wasanii wakubwa watakaotumbuiza katika tamasha hilo linalotarajiwa kukutanisha maelfu ya mashabiki wa muziki. Atapanda jukwaani sambamba na mastaa wengine akiwemo Mbosso, Benson (BNXN), G Nako na Habza.
Tamasha la CRDB IMBEJU Sauti Moja Concert linatajwa kuwa moja ya matukio makubwa ya burudani mwaka huu, likiwa na lengo la kuunganisha mashabiki wa muziki kutoka ndani na nje ya nchi kupitia jukwaa moja.
Kwa mujibu wa waandaaji, maandalizi yote yamekamilika huku mashabiki wakihimizwa kujitokeza kwa wingi kushuhudia burudani ya kiwango cha kimataifa kutoka kwa wasanii hao.
Ijumaa ya Agosti 14 ndiyo siku ambayo Dar es Salaam itageuka kitovu cha burudani, huku Trey Songz akitarajiwa kuwa miongoni mwa mtoa burudani kubwa ya tamasha hilo.




