Tanzania ni salama katika michezo
DAR ES SALAAM: SERIKALI imesema itaendelea kuungana na mataifa mengine Duniani kwenye juhudi za kukabiliana na mbinu haramu na dawa zinazopigwa marufuku michezoni kwa lengo la kusaidia kuleta maendeleo yenye tija kwa jamii.
Kaimu Mkurugenzi wa Michezo nchini,Tamba Boniface ameyasema hayo kwenye semina ya kimatifa ya kupinga matumizi haramu ya dawa michezoni jijini Dar es Salaam.
Amesema Tanzania kuwa wenyeji wa Semina hiyo ya Kimataifa iliyohudhuria na mataifa 13 huku Sita wakiwasili nchini na saba wakiendelea kwa njia ya mtandao.
Mkurugenzi huyo amesema mafunzo hayo ni manufaa kwa Taifa katika kipindi ambacho nchi inajiandaa na uwenyeji wa michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
“Tanzania imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha inazalisha wanamichezo wenye uwezo wa kushindana kihalali, kuepuka kashfa za kutumia madawa ya kuongeza nguvu na mbinu haramu,” amesema Tamba.
Naye Katibu Mtendaji wa Bazara la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha amesema mafunzo hayo ya kimkakati yana lengo la kutoa elimu kwa wanamichezo wote kuhusu kupiga vita matumizi ya mbinu haramu na dawa michezoni.