Tetesi

Simba yatua kwa Kocha ‘Msauzi’

AFRIKA KUSINI:BAADA ya kupitia wasifu wa makocha mbalimbali, uongozi wa Simba umejiridhisha na uwezo wa Steve Komphela wa Afrika kusini kurithi mikoba ya Abdelhak Benchikha.

Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari Steve Komphela ambaye kwa sasa anafundisha klabu ya Golden Arrows inayoshiriki Ligi kuu ya Afrika Kusini, anatajwa kuwa mrithi sahihi wa nafasi ya Benchikha ambayo ilikuwa ikikaimiwa na Juma Mgunda.

Mtoa habari huyo amesema Simba wameingia makubaliano ya awali na kocha huyo ili aje kukinoa kikosi cha Simba kwa msimu ujao kwani wamepania kuja kivingine.

“Suala la kocha sasa limeshafungwa tayari tumemalizana na Steve na anakuja kuchukuwa nafasi ya Benchika, atakuwepo timu ikienda ‘pre season’,” amesema mtoa habari huyo.

Ametutonya kuwa hata suala la usajili amekuwa akishirikiana na watu waliopewa jukumu hilo kulingana na jinsi mapungufu ya timu hiyo alivyoona katika michezo mbalimbali.

Kocha huyo mwenye CV nzito amewahi kuwa kocha mkuu wa Mamelodi Sundowns na kocha msaidizi chini ya makocha wakubwa kama Pitso (Mosimane) na Mokwena (Rhulani) CV hiyo imewavutia zaidi Simba hadi kufikia hatua ya kumtaka haraka.

Ni muumini wa mfumo wa 4-4-2 , amefundisha kama kocha Mkuu Golden Arrows, 2023/24 (Julai4- Feb 19-2024), Moroka Swallows, Oktoba 24, 2022/23: Mamelodi Sundowns, (Kocha Msaidizi), 2020/21, Mamelodi Sundowns, Kocha Mkuu.

Kocha huyo, kwa wakati tofati amewahi kuwa kocha Mkuu wa vilabu kama, FS Stars, Platnum Stars, Afrika ya Kusini chini ya umri wa miaka 20, Dynamos FC na Maning Rangers.

Spotileo leo lilimtafuta Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally ambaye amesema uongozi haujampa taarifa kamili na anatambua mchakato wa utafutaji kocha unaendelea.

“Mchakato wa kutafuta kocha unaendelea na upo chini ya Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Mohammed Dewji na timu yake maalum tunatarajia kupata mwalimu mwenye vigezo,” anasema Ahmed.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button