Shabiki matatani kwa ubaguzi
PALMA, SPAIN: Shabiki wa Klabu ya soka ya Mallorca inayoshiriki ligi kuu ya Hispania Laliga amehukumiwa mwaka jela na kutoingia kwenye viwanja vya michezo kwa miaka mitatu kwa ubaguzi wa rangi dhidi ya Vinicius Junior wa Real Madrid na Samuel Chukwueze wa AC Milan wakati huo akiichezea Villarreal ya nchini Hispania.
Shabiki huyo ambaye jina lake halijawekwa wazi amepewa adhabu hiyo baada ya kuandika barua ya kuomba radhi kwa Vinicius kwa kitendo chake hicho cha ubaguzi alichotenda katika uwanja wa klabu ya Mallorca wa Son Moix stadium Februari 5 2023
Katika mchezo huo ambao Real Madrid ilipoteza kwa bao 1-0 mashabiki wa Mallorca walisikika kwenye video ambazo pia zilitumika kama ushahidi wakimwita Vinicius Jr ‘Nyani wa Kibrazil’ kitendo ambacho kiliathiri uchezaji wa winga huyo wa kushoto wa Real Madrid.
Hukumu hiyo imetolewa leo na mahakama ya mji wa Palma nchini Hispania baada ya kujiridhisha bila shaka juu ya kosa hilo ambalo mtuhumiwa alilitenda kwa wachezaji hao wawili kwa vipindi viwili tofauti.