
KOCHA Msaidizi wa Azam, Kally Ongala amesema anakazi ya kufanya kuimarisha ubora wa washambuliaji wa timu hiyo.
Akizungumza na Spotileo amesema hajafurahishwa namna washambuliaji wake walivyoshindwa kuzitumia nafasi nyingi walizotengeneza kwenye mchezo dhidi ya Yanga.
“Nimefurahi ushirikiano wao lakini sijafurahishwa na kiwango, tumepata nafasi nyingi katika vipindi vyote hawajatumia hata moja,” amesema Kally.
Ongala amesema kulimaliza hilo amepanga kuwaongezea muda wa mazoezi akiamini itawasaidia kuongeza umakini na kutimiza majukumu yao ipasavyo.
Mabao yote mawili ya Azam katika mchezo na Yanga yalifungwa na mabeki wa kati Daniel Amoah na Malickuo Ndoye.